Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA- ZNZ) kimetoa mafunzo ya siku mbili kwa Wahamasishaji Jamii 60 wa Unguja ikiwa ni sehemu ya programu ya kuimarisha uongozi kwa wanawake (SWIL) wenye lengo la kujenga jamii yenye usawa wa kijinsia kwa kuwawezesha wanawake kushika nafasi katika ngazi za maamuzi.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo yenye jitihada za kuimarisha ushiriki wa Wanawake kwenye uongozi na kukuza haki za kidemokrasia , Mkuu wa kitengo cha Mawasiliano TAMWA ZNZ, Saphia Ngalapi amesema watekelezaji wa programu wana imani na wahamasishaji waliopatiwa mafunzo na kuwa watakuwa mabingwa wa kuhamasisha jamii juu ya haki za wanawake kushiriki katika uongozi.

Amesema, “kupitia timu hii, tunatarajia mabadiliko katika kutoa elimu kwa jamii kuhusu haki ya demokrasia na uongozi kwa wanawake ili kufikia 50% kwa 50% katika ngazi za maamuzi, jambo litakalochangia kuleta maendeleo endelevu kwa wote.”

Naye Afisa Ufuatiliaji na Tathmini TAMWA ZNZ, Mohamed Khatib, aliwasisitizia wahamasishaji hao juu ya umuhimu wa kazi yao katika kukuza nafasi za wanawake katika uongozi.

“Tufahamu kuwa hili jambo la kuelimisha jamii si ajira bali ni kazi ya kujitolea kuhakikisha matarajio ya wanawake kushika nafasi za uongozi yanafikiwa kwa kubadilisha mitazamo ya jamii, uchaguzi wa 2025, tunataka tuone wanawake wanashika nafasi za uongozi kuanzia ngazi za shina hadi Taifa kwani uwezo huo wanao,” alifafanua Khatib.

Kwa upande wake Mkufunzi ni mafunzo hayo ya siku mbili, Asha Abdi aliwahimiza wahamasishaji jamii kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha malengo ya mradi huu yanafikiwa.

Ukhty Amina Salum ambae ni kiongozi wa dini na mwanaharakati wa siku nyingi ameeleza shukrani zake kwa kuchaguliwa kuwa sehemu ya wahamasishaji wa jamii.

Alisema, “nafurahi kuwa miongoni mwa wahamasishaji wa jamii, dhamana hii nitaibeba na kuhakikisha jamii inahamasika na kuachana na dhana potofu juu ya uwezo wa mwanamke na maamrisho ya dini kuhusiana na wanawake kushiriki katika uongozi.

Awali Haji Khamis Haji kutoka Mkoa wa Kaskazini Unguja alisisitiza kuwa elimu aliyoipata itamsaidia kuhamasisha jamii katika mkoa wake kutambua haki zao za kidemokrasia na kuongeza wanawake katika nafasi za uongozi.

Mafunzo haya yanaashiria jitihada za TAMWA- ZNZ kwa kushirikiana na Jumuiya ya Wanawake Wenye Ulemavu Zanzibar (JUWAUZA), Jumuiya ya Mazingira, Jinsia na Utetezi Pemba (PEGAO) Jumuiya ya Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA).

Yameshirikisha pia Ubalozi wa Norway katika kuwaandaa wanawake wenye nia ya kugombea nafasi za uongozi kuelekea uchaguzi wa 2025, huku wakilenga kuongeza idadi ya wanawake katika ngazi za maamuzi visiwani Zanzibar.

Mafunzo hayo pia yamejumuisha wawakilishi kutoka makundi mbalimbali ya kijamii ikiwemo viongozi wa dini, watu wenye ulemavu, wanaharakati wa kupinga vitendo vya udhalilishaji na wanaume wa mabadiliko.

Uzinduzi Mradi wa Umeme Rusumo Februari 2025
Achana na ishu ya Gamondi yafahamu mambo 5 yanayoikumba Yanga kwa sasa