Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amemwakilisha Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Phillip Mpango kufungua mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Mashirika ya Umma nchini SHIMMUTA na kuagiza mashirika kuondokana na visingizio visivyo na msingi ili kutimiza azma ya mashindano hayo.
Dkt. Biteko ametoa maelekezo hayo Jijini Tanga ambapo amesema kumekuwa na visingizio vya kuwakosesha watumishi wa umma kushiriki mashindano ilhali ni suala linalofahamika na liko kwenye kalenda ya kila mwaka ya mashirika husika.
“Utaratibu huu wa kukubaliana jambo lakini jambo tulilokubaliana halifanyiki inatufanya tukose uhalali wa kuwasimamia wengine, nilitaka kujua kwanini hatupeleki washiriki katika mashindano haya. Kama tunaona mashindano haya sio ya muhimu ni bora tuondokane nayo tufanye jambo lingine,” amesema Dkt. Biteko.
Amewataka viongozi wa SHIMMUTA kuwatembelea waajiri na kuwahimiza waajiri kuwaruhusu watumishi kushiriki katika mashindano hayo, “hakuna jambo linalouma kwamba baadhi ya watumishi wengine wanashiriki na wengine wanapewa visingizio jambo ambalo halikubaliki kwa namna yoyote na sio sawa.”
Amesema SHIMMUTA haina sababu ya kujipongeza kwa kuvunja rekodi ya kupata washiriki ilhali yapo mashirika mengi ambayo viongozi wake hawajatuma washiriki katika mashindano hayo huku akitoa mfano kuwa kujipongeza kwa hatua hiyo ni sawa na kushangilia goli la kujifunga.
Aidha Dkt. Biteko amefafanua kuwa kutekeleza maelekezo ya serikali kuhusu kushiriki katika michezo kutapunguza gharama na kuwaepusha watumishi na magonjwa yasiyo ya kuambukiza sambamba na kuongeza tija na ufanisi kazini.
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dkt. Batilda Burian amewapongeza washiriki na waandaaji wa mashindano hayo na kuwahakishia utayari wa mkoa kuendelea kuboresha mazingira kwa ajili ya kuwezesha ushiriki mzuri zaidi.

Siku ya Choo Duniani: Umiliki wa Choo bora ni hatua
Habari kuu kwenye Magazeti ya leo Novemba 19, 2024