Mkoa wa Njombe umeahidi kushirikiana na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) katika kusambaza mitungi ya gesi ya kupikia13,020 ili Wananchi watumie Nishati Safi na salama.
Hayo yamezungumzwa hii leo Novemba 19, 2024 Mkoani humo na Kaimu Katibu Tawala, Mhandisi Joseph Mutashubirwa baada ya uwasilishwaji wa taarifa ya utekelezaji wa miradi ya REA katika mkoa huo ulifanywa na Mkurugenzi wa Teknolojia Mbadala na Nishati Jadidifu, Mhandisi Advera Mwijage.
“Nawapongeza REA kwa kuendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, nishati hii ni salama na rafiki katika utunzaji wa mazingira yetu pamoja na afya za watumiaji wa nishati safi, ” amesema Mhandisi Mutashubirwa.
Aidha, Mhandisi Mutashubirwa ameihakikisha REA kuwa mkoa huo utatoa ushirikiano na kuwahamasisha wananchi kuchukua mitungi ya gesi ya kupikia ili kuchochea uchumi na kutunza mazingira.
Kwa upande wake, Mhandisi Mwijage amezitaja wilaya zinazonufaika na mradi huo ni pamoja na Wilaya ya Njombe, Makete, Ludewa, na Wanging’ombe.
“Kila wilaya itasambaziwa mitungi ya gesi 3,255 ya kupikia kwa wananchi kupitia kampuni ya Taifa Gas. Tunaendelea kuhamasisha kujitokeza kwa wingi kuchukua mitungi hii inayotolewa kwa bei ya punguzo ya asilimia 50,” ameeleza Mhandisi Mwijage.
Ameongeza kuwa, elimu ya matumizi sahihi ya nishati safi inaendelea kutolewa kwa Watanzania ili kuhamasisha na kuchochea jamii kutumia nishati safi na salama.