Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu amesema tukio la kuanguka jengo la ghorofa nne katika Mtaa wa Mchikichi na Manyema uliopo Kariakoo jijini Dar es Salaam, limetoa somo kwa Serikali kuanza uchunguzi wa kuhakikisha kunakuwa na usalama wa binadamu na mali zao, kwenye magorofa yaliyojengwa Kariakoo.
Rais Samia ameyasema hayo jijini Dar es Salaam, mara baada ya kulitembelea jengo lililoanguka Novemba 16, 2024 na kupewa taarifa kuwa limesababisha vifo vya watu 20 na kudai kuwa ni dhahiri fedha kidogo ndio iliyotumika kujenga jengo hilo kubwa bila kujali madhara yatakayotokea kutokana na kutokuwa imara.
Amesema, “tukio hili limetupa somo kubwa la kuangalia usalama wa majengo yetu katika eneo la Kariakoo, wakati naonyeshwa jengo na nilipoliangalia namna lilivyojengwa kuta zake na nondo zilizotumika bila shaka halikuwa na usimamizi mzuri.”
Rais Samia pia amesema, wakati zoezi la kusafisha eneo hilo likiendelea kuna ulazima kwa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji pamoja na vyombo vingine vya ulinzi na usalama kuendelea kufukua kifusi ili kama kuna miili iliyosalia chini itolewe na ipate heshima ya kusitiriwa.
Aidha, amewashukuru wananchi wote waliofika katika kuwaokoa wahanga badala ya kutaka kuiba, huku akielekeza, mali zote zilizopo katika jengo hilo ziende kuhifadhiwa mpaka zoezi la uokozi na usafishaji wa eneo hilo ukamilike na Wafanyabiashara waende kutambua mali zao na kuzichukua.

Maduka jela miaka 30 kwa kubaka Mtoto mgonjwa
TET yatarajia kuadhimisha miaka 50 Mei 2025