Johansen Buberwa – Kagera.
Mkuu wa Wilaya Karagwe, Julius Laizer ameipongeza Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira – BUWASA, kwa kuendelea na usimamizi wa utekelezaji wa Miradi ya Maji ya Maendeleo wa Kata ya Ihanda, unaogharimu zaidi ya bilion 1.7 utakao nufaisha wanachi 10,500 wa vijiji vitatu ndani ya wilaya hiyo.
Akizungumza wakati alipotembelea mradi huo katika Kijiji cha Ihanda kilichopo Kata Ihanda Wilayani humo hii leo Novemba 20, 2024 amesema kuwa mradi huo utakuwa msaada kwa Wananchi.
Amesema, “nimpongeze mkandarasi pamoja na idara ya Buwasa kwa namna ambavyo mnaendelea kusimamia mradi huu na spidi hii tunaiona inaenda vizuri.”
Awali, akisoma taarifa ya utekelezaji wa Mradi huo Meneja BUWASA Kanda ya Karagwe, Magreth Mnyange amesema mpaka sasa umefikia asilimia 52 za utekelezaji na upo katika hatua ya uchimbaji na ulazaji na ufukiaji wa bomba na usambazaji wa kilometa 14.1 kati ya kilometa 26.9 kwenye Vijiji hivyo.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Ihanda, Ladislaus Kamwangile kwa niaba ya Wananchi wa Kata hiyo amesema awali walikuwa na adha ya kutokuwa na maji safi na Salama lakini sasa wameondokana na tatizo hilo.