Mfumo wa usimamizi wa ununuzi wa umma kielektroniki (NeST) umeshinda tuzo ya “Mfumo Bora Zaidi wa Ununuzi wa Umma Barani Afrika” katika tuzo za African Association for Public Administration and Management (AAPAM), zilizokuwa zikishindaniwa chini ya uangalizi wa Umoja wa Afrika (AU), jijini Kampala, Uganda.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Kampala, baada ya kupokea tuzo hiyo mbele ya mamia ya washiriki wa Mkutano wa AAPAM, Novemba 28, 2024, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), inayosimamia NeST, Dennis Simba, alisema kuwa tuzo hii ni heshima kubwa kwa Tanzania, kwani ununuzi wa umma ni moja ya maeneo yanayotumia asilimia kubwa ya fedha za umma barani Afrika.
“Tuzo hii imetuletea heshima kubwa, kwani tulifika katika tano bora kati ya washiriki 69 na ni sisi pekee ambao tumeingiza mfumo wa ununuzi wa umma na leo umetambulika na kupewa tuzo hii… ni mafanikio makubwa kwa Tanzania na kwa mfumo wetu,” alisema Simba.
Aidha, ameelekeza pongezi za kipekee kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, aliyewezesha kuanzishwa kwa sheria ya ununuzi wa umma ya Mwaka 2023, na kuundwa kwa NeST, mfumo ambao umetambulika Afrika nzima kwamba ni bora wa ununuzi wa umma.”
Simba alisema kwa kuwa mfumo huu umejengwa na wataalam wa Tanzania pekee, PPRA iko tayari kushirikiana na nchi nyingine kuhakikisha kuwa teknolojia hii inawafikia na kusaidia katika mageuzi ya sekta ya ununuzi wa umma barani Afrika.
Kwa upande mwingine, mfumo wa kutoa huduma ya afya kwa jamii nchini Kenya umeshinda tuzo ya jumla, huku Uganda ikikabidhiwa Tuzo Maalum (Special Award) kwa kuwa mwenyeji wa mkutano wa AAPAM.