Boniface Gideon – Tanga.

Vyama vya Siasa vilivyoshiriki Uchaguzi wa Serikali za mitaa wa Novemba 27, 2024 katika Halmashauri ya Jiji la Tanga, vimetoa tamko la pamoja na kupongeza mchakato wa Uchaguzi huo huku vikitoa dosari chache zinazotakiwa zifanyiwe kazi na Tamisemi.

Vyama hivyo ni pamoja na Chama cha Mapinduzi ‘CCM’, Chama Demokrasia na Maendeleo ‘CHADEMA’  na vyama vyengine ni ACT-Wazalendo, CUF, ADC, TLP na NCCR-Mageuzi.

Vyama hivyo vimetoa tamko la pamoja leo Novemba 29 mara baada ya matokeo ya jumla kutangazwa hapo jana ambapo CCM katika Jiji la Tanga kimeibuka kidedea kwakushinda viti vyote vya kuanzia wajumbe na wenyeviti wa mitaa yote.

Wakizungumza na Waandishi wa Habari wakati wa tamko la pamoja, Mussa Mbarouk, Mwenyekiti wa chama cha Wananchi CUF , Wilaya ya Tanga, amesema Uchaguzi huo ulifanyika kwanjia ya amani japo kulikuwa na dosari ndogondogo ambazo zinatakiwa zifanyiwe kazi,

“Mchakato wa Uchaguzi huu ulienda vizuri, tulikuwa tukishirikiana na upande wa Serikali ya Mkoa na Jiji, kulikuwa na dosari ndogondogo ikiwemo majina kutolewa ‘photocopy’ kwahiyo yalikuwa hayaonekani vizuri, lakini hata sisi vyama vya siasa tunatakiwa tukae na tuungane ili yale maeneo yote yenye Wagombea wanaokubalika tumuunge mkono” alisema Mbarouk.

Aliongeza kuwa chama chake pamoja na vyama vyote shiriki katika Uchaguzi huo vimesikitishwa na matokeo ya jumla ambapo hakuna chama cha upinzani kilichoshinda kiti hata kimoja.

“Nimesikitishwa na matokeo ya Uchaguzi huu, kiukweli hakuna chama kilichopata hata kiti cha ujumbe wa mtaa au Uenyekiti,hii haijawahi kutokea, Uchaguzi wa Serikali za mitaa wa 2019 tulipata walau viti 61, lakini safari hii haijawahi kutokea kiukweli,nilazima tujipange vizuri Uchaguzi Mkuu” alisisitiza Mbarouk.

Naye Hemed Bakari mwenyekiti ngome ya vijana ‘Chadema’, amesema Kuna umuhimu mkubwa kwa vyama vya Siasa kuongeza nguvu ya ushawishi kwa wapiga kura.

“Licha ya dosari ndogondogo za Uchaguzi wa Serikali za mitaa, lakini mwamko wa wapiga kura ni mdogo sana,watu wengi walijiandikisha kwa lengo la kurahisisha upataji wa huduma tu,lakini kiukweli bado tunatakiwa tuongeze nguvu kubwa ya ushawishi kwa wapiga kura wetu,hasa kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwakani,” alisisitiza Bakari.

Kwa upande wake katibu wa chama cha Mapinduzi ‘CCM’, Shaban Kalaghe alisema mchakato wa Uchaguzi huo ulienda vizuri na kuwashukuru watu wote waliojiandikisha na kupiga kura.

“Niwapongeze wasimamizi wa Uchaguzi huu, ulienda vizuri tulikuwa na wagombea kwenye mitaa yote na tumeshinda kwa asilimia 100, lakini pia tunawashukuru wenzetu wa vyama vingine kwakukubali matokeo jambo zuri na linaonyesha ukomavu mkubwa wa kisiasa, Uchaguzi huu umeisha sasa tunaenda kufanya kazi lakini pia kujiandaa na Uchaguzi Mkuu, naomba tukashikashirikiane ili tupate viongozi bora watakaotuongoza kwa miaka mitano mingine,” aliongeza Kalaghe

Picha: Rais Samia katika mjadala wa EAC