Johansen Buberwa – Kagera
Watu saba wamefariki dunia na wengine tisa kujeruhiwa baada ya kutokea kwa ajali ya gari eneo la Kihanga lililopo Wilayani Karagwe Mkoani Kagera hii leo Desemba 3, 2024.
Ajali hiyo ilihusisha gari kubwa la mizigo aina ya Scania lenye namba za usajili T 621 AJQ lioiwa na Tela namba T 472 EAQ ambalo liliyagonga magari mengine mawili ya abiria yaliyokuwa yamesimama Toyota Coaster namba T 367 ECP pamoja na Toyota Hiace namba T 976 DGD.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Blasius Chatanda amesema chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa Dereva wa Lori ambaye alikuwa na mwendo kasi kisha kuyagonga magari hayo yaliyokuwa na abiria ambayo yalisimama yakiwa yanakaguliwa na Maafisa kutoka Idara ya Uhamiaji kwenye kizuizi.
Amesema, “katika vifo hivyo saba kuna Wanawake wanne, Mwanaume mmoja na Watoto wawili, kwenye majeruhi kuna Wanaume wanne na Wanawake watano, chanzo ni uzembe, kama ingekuwa mfumo wa breki umefeli asingeumaliza mteremeko na kona zilizo karibu na eneo la ajali, pia kuna vibao vinaonesha simama ukaguliwe.”
Kamanda Chatanda ameongeza kuwa miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya Karagwe na majeruhi wanaendelea kupatiwa matibabu, huku akitoa rai kwa madereva wa vyombo vya moto kuzingatia sheria za usalama za Barabarani na kumtaka Dereva aliyesababisha ajali kujisalimisha kwani alitoroka baada ya tukio.