Kampuni ya Dar24 Media inatarajia kufunga mwaka 2024 kwa staili ya kipekee kwa kuwakutanisha Vijana wa Temeke na kuwaletea Bonanza la Mpira wa Miguu.
Bonanza hilo lililopewa jina la Dar24 Chandimu Cup, litazikutanisha timu nane kuanzia hatua ya robo fainali, nusu fainali na fainali, huku kukiwa na zawadi kedekede kwa timu shiriki.
Aidha, Tamasha hili la kipekee litaanza rasmi Desemba 14 hadi 21, 2024 katika Viwanja vya Chamazi vilivyopo, Mbagala jijini Dar es Salaam.
Meneja wa Dar24 Media, Naomi Tetemeko anawakaribisha wadau mbalimbali kujitokeza na kuungana na familia ya wanamichezo, ili kuwafikia Vijana wa Temeke na maeneo jirani.
Lengo kuu la Tamasha hili ni kuhubiri Amani, kupinga matumizi ya Dawa za Kulevya, kupinga Ukatili wa Kijinsia na namna bora ya kupambana na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi.