Serikali ya Tanzania itaendelea kuchukua hatua kali kwa taasisi zote ambazo zinazotoa huduma za fedha kinyume cha sheria kwa kutoa mikopo umiza maarufu kama kausha damu kwa kuwakandamiza wananchi.
Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba wakati akizindua jukwaa la kwanza la Wadau wa Sekta ya Fedha kwa mwaka 2024 leo jijini Dar es Salaam Desemba 10, 2024 amesema taasisi hizo zimekuwa zikiwaumiza wananchi kwa kutoa mikopo yenye riba kubwa pamoja na kupanga njama za kuwafilisi wale ambao wanajua wazi hawatoweza kulipa mikopo hiyo.
“Ni vema wadau wa sekta ya fedha wawaelimishe wananchi kuhusu umuhimu wa kutumia benki kupata mikopo pamoja na kutunza fedha zao kwa kuwa kutunza fedha benki ni utaratibu wa kisasa wa uendeshaji wa uchumi,” amesema Dkt Nchemba.
Waziri Nchemba amesema pamoja na kazi nzuri iliyofanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ya kukusanya kodi kwa weledi na kwa kufuata sheria bado wananchi hawajapa uelewa vizuri kuhusu umuhimu wa kutunza fedha zao benki.