WAF, Dodoma.

Waziri wa Afya, Jenista Mhagama amesema kurejeshwa kwa Toto Afya Kadi kutaleta matumaini mapya na uelekeo thabiti wa Bima ya Afya hususan kwa kundi la watoto ambalo linahitaji uangalizi wa pekee.

Mhagama ameyasema hayo Jijini Dodoma, wakati akizindua vifurushi vitatu vya vya Bima ya Afya kikiwepo cha Toto Afya Kadi.

Waziri Mhagama amesema Mpango huo wa Toto Afya Kadi utasaidia familia za wananchi hasa zile zenye watoto wenye changamoto za kiafya.

Waziri Mhagama ameongeza kuwa mpango wa sasa wa usajili wa Toto Afya Kadi utafanyika pia kwa mtoto mmoja mmoja iwapo itatokea mtoto husika hayupo shule, hii ni hatua kubwa na yakujivunia katika sekta nzima ya afya.

“Kila tunapokutana kwa ajenda ya ya Afya, tujue tunazungumzia usalama wa Taifa, maendeleo endelevu na uchumi wa nchi,” amesema Mhagama.

Mbali na kifurushi cha Toto Afya Kadi kilichozinduliwa leo, vifurushi vingine ni Ngorongoro chenye huduma 445 na Serengeti chenye huduma 1,815 ambavyo vyote vimelenga kuhudumia watanzania.

Waziri Mhagama amesema mara baada ya uzinduzi wa vifurushi hivyo ajenda iliyopo mbele ni ubora wa huduma, huku akiwataka watoa huduma kuibeba ajenda hiyo na kutoa huduma zenye tija kwa maslahi ya umma wa watanzania ili waone umuhimu wa Bima na ifikapo 2030 Tanzania iwe imetimiza malengo ya kidunia.

Amesema Serikali imefanya uwekezaji mkubwa wa Vifaa Tiba na Dawa ambapo kwa sasa upatikanaji wa dawa ni wastani wa asilimia 86 ambayo imewezesha wananchi kunufaika na huduma hizo.

“Takriban vituo 9,826 nchi nzima, kati ya vituo hivyo, vituo 7,366 (sawa na 75%) ni vya Serikali, vituo 1,375 (sawa na 14%) vinamilikiwa na watu binafsi, vituo 1,006 (sawa na10.2%) vinavyomilikiwa na mashirika ya dini na vituo 79 (sawa na 0.8%) vinamilikiwa na mashirika ya Umma. Vilevile kuna jumla ya kliniki 987 na Maabara 1,590,” amefafanua Mhagama.

Akizungumza kwenye hafla hiyo Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na UKIMWI, Elibariki Kingu ameishukuru Serikali kwa kutekeleza maagizo ya Bunge huku akiahidi kuendelea kutoa ushirikiano katika kulisemea suala la Bima

Ajali ya Lori, Coaster yauwa 14 Morogoro
Wanafunzi 809 wapangiwa Shule za Vipaji maalum