Mtuhumiwa wa unyang’anyi wa kutumia silaha, Atanasio Malenda (30), ambaye aliwauwa Askari wawili kwa risasi Koplo Jairo Boniface Kalanda na PC Alfred John naye amefariki Dunia.

Taarifa ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, George Katabazi ambayo imetolewa hii leo Desemba 18, 2024 imeeleza kuwa tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia hii leo majira ya saa saba usiku katika Kijiji cha Msagali kilichopo Wilaya ya Mpwapwa Dodoma.

“Mnamo tarehe 18.12.2024 majira ya saa saba usiku huko katika Kijiji cha Msagali Wilaya ya Mpwapwa Mkoa Wa Dodom Askari Polisi D/Cpl. Jairo Boniface Kalanda na Pc. Alfred John walifariki dunia katika mapambano ya risasi wakati wakimkamata Mtuhumiwa,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.

Marehemu Atanasio ambaye alikuwa Mkulima alikuwa akitafutwa baada ya kumjeruhi Yohana Lameck na kumpora kiasi cha Tshs Milioni mbili na alifariki dunia akiwa anapatiwa matibabu Hospitali ya Wilaya ya Mpwapwa kutokana na majeraha aliyoyapata wakati wa mapambano hayo.

Kamanda Katabazi ameeleza kuwa, Askari Polisi hao wakiwa na wenzao walipata taarifa kuwa mtuhumiwa huyo aliyekuwa anatafutwa yuko nyumbani kwake katika Kijiji Cha Msagali na walifika Kijijini hapo na kutafuta uongozi wa kijiji na kuelekea nao nyumbani kwa mtuhumiwa huyo.

“Mtuhumiwa huyo alitoka ndani na kuanza kuwashambulia askari na katika majibizano hayo ndipo vikatokea vifo hivyo. Aidha katika majibizano hayo askari D/cpl. Msuka na raia mmoja anaefahamika kwa jina la Masima Nyau wamejeruhiwa na wanaendelea na matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Mpwapwa.

Kapinga atangaza fursa za uwekezaji Nishati Saudi Arabia
CBT yachangia Tani 1,900 za Salfa ya Maji ya Korosho Pwani