Polisi nchini Zambia inawashikilia watu wawili wamekamatwa kwa madai ya kupanga njama za kumdhuru Rais wa Zambia, Hakainde Hichilema kwa njia za ushirikina.
Taarifa ya Msemaji wa Polisi Nchini humo, Rae Hamoonga iliwataja watuhumiwa hao kiwa ni Jasten Mabulesse Candunde, na Leonard Phiri ambao wanadaiwa kutumwa na Nelson Banda, mdogo wa mbunge anayekabiliwa na tuhuma za wizi Jay Jay Banda, kumroga kiongozi huyo.
Madai yanayowakabili ni kula njama za kufanya uchawi, kumiliki hirizi na ukatili kwa wanyama baada ya kukutwa na hirizi za aina mbalimbali zikiwemo kinyonga hai.
Hamoonga amesema watuhumiwa hao walikiri kula njama hizo na walikuwa wamekubaliana walipwe kiasi cha dola 7,400 za Marekani baada ya kufanikisha zoezi hilo.