Moja kati ya taarifa zilizowahi kutikisa ulimwenguni ni lile tukio la Mzee mmoja wa nchini Bangladesh, Shahjahan Bhuiyan ambaye mwaka 1991 alihukumiwa na Mahakama kifungo cha miaka 42 jela kwa kosa la kumuua mtu bila kukusudia, na kuachiliwa huru wiki moja baadaye.
Kilichoshangaza si mzee huyu kuachiliwa huru kwa kuuwa mtu mmoja, bali kuachiliwa baada ya kuwaua wafungwa wengine 26 akiwa gerezani na kuzua gumzo kubwa nchini humo na Ulimwenguni kiujumla, huku raia wengi wakitaka arudishwe tena gerezani la sivyo watajua la kufanya.
Lakini Serikali kupitia Idara ya Magereza nchini humo, ilitangaza sababu za kumuachia huru Mzee huyo, ikisema alisaidia kazi ya kuwanyonga wafungwa hao 26, ambao walikuwa wamehukumiwa kunyongwa na Mahakama za nchini humo, kazi ambayo ilishindwa kutekelezwa na wahusika.
Iliarifiwa kuwa, Mzee huyo hakulazimishwa bali baada ya Idara ya Magereza kusema hakuna aliye tayari kuifanya kazi hiyo ya kuwanyonga wafungwa hao waliokaa muda mrefu, alijitolea kwa moyo mkunjufu na kupelekea kupata tena uhuru wake, kwa ahadi kuwa ataenda kuwa raia mwema kwa jamii.