Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam, limefanikiwa kuwapata Watoto wawili wa miaka 5 na wa miaka 4 wa kike na wa kiume, wote wa familia ya Mohamed Kasim mkazi wa Tandika Temeke, ambao waliripotiwa kupotea.
Taarifa ya Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro imeeleza kuwa tukio hilo lilitokea Januari 12, 2025 ambapo pelelezi ulianza mara moja na kubaini kuwa Binti wa kazi za ndani kwa kushirikiana na Mganga wa kienyeji walipanga njama na kuiba watoto hao.
“Wamepatikana Januari 14, 2025 nyumbani kwa mtuhumiwa Abdulkanm Shariff (43), Mganga wa Kienyeji Mkazi wa Kimara Baruti Ubungo. Afya za watoto hao baada ya vipimo hospitali imeonesha ni nzuri,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Aidha, Muliro kupitia taarifa iyo ameeleza kuwa mahojiano ya kina na watuhumiwa yanakamilishwa ili kubaini nini kiini na malengo ya tukio hilo na kwamba wote waliohusika katika tukio hilo watafikishwa kwenye mamlaka zingine za kisheria kwa hatua zaidi.