Baraza la Taifa la Ujenzi – NCC, linaendesha zoezi la kufanya mapitio ya rasimu ya kanuni za majenzi na maoni yaliyotolewa na Benki ya Dunia kuhusu kanuni hizo, zoezi litakalofanyika kwa wiki mbili likiongozwa na timu ya wahandisi chini ya usimamizi wa Mtendaji Mkuu wa NCC, Dkt. Mhandisi Matiko Mturi.

Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Mhandisi Geofrey Mwakasenga ameeleza NCC lina jukumu la kuandaa, kuratibu, na kusimamia maendeleo ya viwango, kanuni, na miongozo ya sekta ya ujenzi nchini, ikiwa ni moja ya misingi ya sheria ya ujenzi ambayo pia Baraza linasimamia.

Amesema, kanuni hizo pia zinatarajiwa kuwa muongozo wa Kitaifa wa kusimamia usalama wa majengo, usalama wa watumiaji, na kuhakikisha majengo yanazingatia utunzaji bora wa mazingira, ndani na nje ya jengo, huku akitoa wito kwa wadau wa sekta ya ujenzi kutumia kanuni hizo mara zitakapokamilika, akibainisha kuwa zitaleta manufaa makubwa kwa kupunguza athari zinazotokana na ujenzi usiozingatia viwango.

“Tunaomba wadau wote wa tasnia ya ujenzi kutumia kanuni hizi mara zitakapokamilika ili kupunguza au kuondoa athari zinazoweza kujitokeza katika ujenzi,” amesisitiza Mhandisi Mwakasenga.

Kwa upande wake, Msanifu Majengo, Arch. Mariahildergard Byarufu amesema kuwa kanuni hizi zitasaidia kuimarisha viwango vya ujenzi na kuhakikisha mazingira rafiki kwa watumiaji wote, wakiwemo wenye mahitaji maalum.

“Kupitia kanuni hizi, majengo yatakuwa na nafasi zinazokidhi viwango vinavyotakiwa, na kuwezesha kundi hili kutumia majengo bila kuhitaji msaada wowote,” alisema.

Copa Del Rey:Real Madrid yatinga robo fainali kwa kishindo
Maisha: Kama zali, mrembo aukwaa utajiri