Ugonjwa wa matende ni aina ya ugonjwa unaosababisha ngozi na  tishu zilizo chini ya ngozi ya  mwanadamu kuwa nene (thickening of skin and underlying tissue).Ugonjwa huu  huathiri  miguu, mikono, figo,  korodani  na kusababisha korodani  kuvimba na kuwa kubwa sana.

Inakisiwa watu milioni 120 duniani wana maambukizi ya ugonjwa huu ambapo kati yao milioni 40 wamepata madhara makubwa kutokana na ugonjwa huu.Kati ya hawa walioathirika theluthi moja huapatikana katika bara la Afrika, theluthi moja nyingine hupatikana India, na kiwango kilichobakia hupatikana katika  visiwa vya Pacific, Marekani na Asia ya kusini.

Ugonjwa wa matende husababishwa  na vimelea aina ya minyoo (parasitic worm) vinajulikana kama Wuchereria bancrofti, Brugia malayi, B. timori ambavyo huenezwa na mbu jike aina ya  culex quinquefasciatus mosquitoes na jamii fulani ya mbu dume (Anopheles species) wakati minyoo aina ya  Brugia roundworms huenezwa mbu wanaojulikana kama  Mansonia mosquitoes. Mbu hawa hueneza ugonjwa huu kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwengine.
Aina nyingine ya ugonjwa wa matende inayojulikana kama nonparasitic elephantiasis au podoconiosis ambayo haisababishwi na vimelea vyovyote hupatikana katika nchi za Afrika Mashariki (Kenya, Uganda, Tanzania, Rwanda, Burundi) Sudan, Egypt na Ethiopia. Asilimia 6 ya maambukizi ya aina hii ya podoconiosis hupatikana nchini Ethiopia.

Nini hutokea baada ya maambukizi?

Kwa kawaida mtu aliyeambukizwa ugonjwa huu huwa na mabuu (larvae) kwenye mfumo wa damu mwilini mwake wanaojulikana kama microfilariae. Mabuu haya husafiri kutoka kwenye mfumo wa damu hadi kwenye mfumo mwingine unaojulikana kama mfumo wa limfu (lymphatic system).
Kukua kuwa minyoo kamili (adult worms) ambayo huziba mfumo huu wa limfu ambao unategemewa sana katika kuweka uwiano sawa  wa maji (fluid balance) kati ya mfumo wa damu na tishu ndani ya mwili na husaidia kuupa mwili kinga dhidhi ya magonjwa mbalimbali. Minyoo hii huishi kwa miaka minne hadi sita na katika uhai wake huzaa mamilioni ya mabuu (microfilariae)  mengine wakati ikiwa kwenye mfumo wa damu.

Mbu huenezaje ugonjwa huu?

Mtu ambaye ameambukizwa ugonjwa huu huwa na mabuu kwenye mfumo wake wa damu na anapongatwa na mbu ambawo wanauwezo wa kuchukua mabuu haya  ambayo  huendelea kukua na kufikia hatua ya kuambukiza mtu mwingine ndani ya mwili wa mbu.Kwa kawaida, ukuaji huu wa mabuu ndani ya mwili wa mbu huchukua wiki moja hadi tatu na baada ya kukua na kufikia hatua ya kuambukiza mtu mwingine.
Mabuu haya husogea mpaka kwenye sehemu ya mdomo wa mbu ambayo ndio huwa humng’ata mtu wakati mbu anapofyonza damu kutoka kwa mtu. Mbu mweye mabuu kwenye mdomo wake anapomngata mtu ili kufyonza damu, ndipo mabuu haya yanapoingia kwenye mwili wa mtu na hivyo kusababisha maambukizi ya ugonjwa huu.

Dalili za ugonjwa huu ni zipi?

• Dalili kubwa ya ugonjwa huu ni kuvimba sehemu ya chini ya mwili yaani kwenye miguu na vidole.Pia mtu anaweza kuvimba sehemu ya mikono au mkono wote pamoja na vidole vya mkononi. Wengine huvimba kwenye korodani (wanaume).
• Kuhisi uzito na kukamaa kwa mikono au miguu kutokana na uvimbe uliopo.
• Kutoweza kutumia kiungo husika kilichovimba.
• Maumivu au kutohisi vizuri kwenye mikono au miguu.
• Kupata maambukizi ya mara kwa mara kwenye sehemu iliyovimba.
• Ngozi kuwa nene na ngumu kwenye mikono au miguu.

Dalili nyingine ni pamoja na

  • Homa
  • Maumivu ya kichwa
  • Maumivu kwenye jointi na mifupa
  • Kutapika
  • Vidonda kwenye mikono au miguu
  • Mistari ya rangi nyekundu inayoonekana kwenye mikono au miguu (red streaks)

Vipimo vya uchunguzi

• Blood examination under microscope – Kipimo cha kuangalia damu kwenye hadubini  ili kuangalia kama kuna mabuu ya ugonjwa huu wa matende.Kwa wale ambao wana ugonjwa huu kwa muda mrefu, mabuu hayaonekani kwenye damu kwani tayari yatakuwa yameshaingia kwenye mfumo wa limfu. Hivyo, kutoonekana kwa mabuu kwenye damu kwa kutumia hadubini si kigezo cha kusema kwamba mgonjwa hana ugonjwa huu wa matende.
• Vipimo vyengine vinavyoweza kutumika ni pamoja na CT Scan, MRI, Doppler Ultrasound, Radionuclide Imaging ili kuweza kutofautisha ugonjwa huu na magonjwa mengine yanayosababisha kuvimba kwa miguu au mikono kama saratani za  aina mbalimbali, kuganda kwa damu kwenye mishipa ya damu (blood clot) na kadhalika.
• Kwa wale wenye kuvimba korodani, ni muhimu kwa daktari  kuchukua kipimo kwa kukwangua sehemu husika kisha kuchanganya na potassium hydroxide na kutazama kwenye hadubini kama kuna dalili (Meddler bodies, sclerotic bodies)  za ugonjwa wa fangasi unaojulikana kama chromobalstomycosis  (unaosababishwa na fangasi aina ya Fonsecaea pedrosoi, Phialophora verrucosa, Cladosporium carrionii, au Fonsecaea compacta). Pia ukungu huu huweza kuoteshwa maabara ili kuangalia kama kuna fangasi aina yoyote ile niliyotaja hapo juu watakaota.

Tiba ya ugonjwa wa matende ni nini?

Tiba ya ugonjwa wa matende hutegemea na sehemu husika. Kwa wagonjwa walio katika jangwa la sahara, tiba ni dawa aina ya albendazole pamoja na ivermectin. Kwa wagonjwa waliopo sehemu nyingine duniani tiba huusisha matumizi ya albendazole pamoja na diethylcarbamazine.
Kusafisha sehemu iliyoathiriwa na ugonjwa wa matende mara kwa mara husaidia kupunguza dalili na viashiria vya ugonjwa huu.
Kwa wale waliovimba korodani kutokana na ugonjwa wa matende, tiba yake ni upasuaji.Wakati mwingine, kama mgonjwa atakuwa amevimba sana korodani, basi baada ya kufanyiwa  upasuaji wa kawaida, atahitaji kufanyiwa upasuaji kurekebishwa ngozi yake (plastic surgery).
Katika utafiti uliofanywa na chuo cha Liverpool school of tropical medicine mwaka 2005, umeonyesha dawa ya antibiotiki hususan doxycyline inaweza kutumika kutibu ugonjwa huu wa matende kutokana na  minyoo (adult worms) kuwa na bakteria aina ya wolbachia wanaoishi ndani ya minyoo hii, hivyo dawa hii hutibu kwa kuua bakteria hawa na kusababisha minyoo hii kufa, na kuondosha kabisa microfilariae kwenye damu ya mgonjwa na  hivyo mgonjwa kupona. Dawa hii hutumika kwa muda wa wiki 8. Hata hivyo, kama mgonjwa atakuwa na mabuu ndani ya mfumo wake wa limfu, basi itakuwa vigumu kwake kupona. Utafiti zaidi unahitajika ili kuwa na uhakika zaidi juu ya dawa hii kutibu ugonjwa huu.

Kinga ya ugonjwa wa matende ni nini?

• Shirika la afya duniani (WHO) limeanzisha jitihada za kutokomeza ugonjwa huu wa matende ifikapo mwaka 2020.
• Matumizi ya  dawa aina ya albendazole kwa wale walio katika hatari kupata ugonjwa wa matende unaosababishwa na vimelea.
• Kuvaa viatu wakati wa kutembea nje ili kujikinga kupata maambukizi ya aina ya podoconiosis.
• Kuosha miguu na mikono kwa kutumia maji na sabuni
• Kuosha miguu kila siku kwa kutumia antiseptic (bleach).
#Dkt. Khamis H. Bakari (MD PhD)

Dakika za jioni zimerudisha heshima ya Manchester United ,Amad Diallo awa gumzo
Wananchi Vitambulisho vyenu vipo tayari - NIDA