Wakati klabu ya Yanga kihitaji alama tatu iweze kutinga hatua ya robo fainali ya ligi ya mabingwa Afrika ,hali ni tofauti kwa wapinzani wao MC Alger. Yanga wana alama 7 kwenye msimamo wa kundi A wakishika nafasi ya tatu.Wanapaswa kushinda dhidi ya Mc Alger wenye alama 8 na jambo hilo linawezekana kabisa ndani ya Dimba la Benjamin Mkapa.
Yanga walianza vibaya mechi mbili za kwanza dhidi ya Al Hilal mchezo waliopoteza kwa mabao 2-0 dimba la Benjamin Mkapa kisha ikapoteza kwa mabao 2-0 dhidi ya Mc Alger mchezo uliopigwa nchini Algeria. Sare ya mabao 1-1 dhidi ya TP Mazembe raundi ya 3 ilirejesha matumaini kwa Yanga na mchezo wa raundi ya 4 Yanga waliibuka na ushindi wa mabao 3-1 uliirejesha klabu hiyo kuwania kufuzu robo fainali. Ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Al Hilal nchini Mauritania ulikamilisha ndoto ya kuelekea robo fainali kibabe.
Tathmini ya mchezo mgumu dhidi ya MC Alger
Mchezo huu ni fainali kwa klabu hizi mbili.Yanga akiwa hapa nchini anapaswa kushinda mchezo huo kwa namna yoyote,ikitokea yanga amepata sare au kufungwa basi safari yao ya kushiriki Ligi ya mabingwa itakuwa imeishia hapo na watapaswa kurejea nyumbani kujipanga kwa msimu ujao.
MC Alger anataka kufuzu akiwa ugenini na anaamini ataondoka walau na sare katika mchezo huo ili kufikisha alama 9 na kuwa nyuma ya vinara wa kundi kwa alama 1. Ikitokea ameshinda mchezo huo basi atatimiza alama 11 na hapo atamwangalia mpinzani wake Al Hilal amepata matokeo gani ili kutambua nani atamaliza kiongozi wa kundi lao.
Rekodi zinaonyesha kwamba msimu huu Mc Alger akiwa ugenini amecheza michezo 2 na alipata sare dhidi ya Al Hilal ya bao 1-1 na sare ya 0-0 dhidi ya Tp Mazembe wakati mechi za nyumbani aliishinda 2-0 dhidi ya Yanga ,1-0 dhidi ya Tp Mazembe na kupoteza 1-0 dhidi ya Al Hilal. Timu hiyo imefunga mabao 4 na kuruhusu 2.
Yanga kwa msimu huu wamecheza michezo 2 ya nyumbani wakishinda mabao 3-1 dhidi ya Tp Mazembe na kufungwa 2-0 dhidi ya Al Hilal.Kwa upande wa ugenini Yanga wameshinda mchezo 1,sare 1 na kupoteza 1. Wakiruhusu kufungwa mabao 6 wakati wao wakifunga mabao 5.
Nini kifanyike Yanga ushinda mchezo huo?
Yanga wapo katika ubora wa hali ya juu kwa sasa, Katika michezo mitano iliyopita ya Ligi kuu na Ligi ya mabingwa Afrika Yanga wameshinda mechi zote kwa kufunga jumla ya mabao 19 na kuruhusu mabao 3 pekee. Kwa mwenendo huu inadhihirisha ubora wa safu zote ndani ya kiwanja.
Kocha Ramovic hatakuwa na kazi kubwa ya kukiandaa kikosi chake ila kama ningepata nafasi ya kuandaa kikosi cha kuanza katika mchezo huo basi ningeanza na Djigui Diarra,Yao Kwasi,Boka ,Ibrahim Bacca,Dickson JOB,Khalid Aucho,Maxi Nzengeli,Mudathir Yahya,Clement Mzize,Pacome Zouzoua na Aziz Stephanie Ki. Benchi langu lingekuwa na watu kama Clatous Chama,Prince Dube,Duke Abuya,Kibabage,Kibwana Shomari na Jonas Mkude.
Yanga wanapaswa kuutawala mchezo huu kama wafanyavyo siku zote,Mc Alger ni wagumu kufungika hasa wanapocheza uwanja wa ugenini Hivyo Yanga wanapaswa kucheza kwa kushambulia muda w0te.Ikumbukwe katika mechi 2 za ugenini wameruhusu bao 1 pekee pia wanaelewa kwamba sare ya aina yoyote itawapeleka robo fainali.
Rekodi ni kikwazo kwa Yanga
Yanga na Mc Alger wamekutana mara 3 tangu msimu wa 2017.Timu hizo zilikutana hatua ya makundi ya kombe la shirikisho kwa mechi 2 ambazo Yanga aliibuka na ushindi wa bao 1-0 uwanja wa Benjamin Mkapa na kufungwa 4-0 Pale Alger Algeria.Timu hizo zimekutana tena msimu huu na Yanga kupoteza kwa mabao 2-0 hatua ya makundi ya ligi ya mabingwa Afrika.