Jeshi la Polisi Mkoani Shinyanga, limelazimika kufukua mwili wa Mwanamke mmoja aitwaye Asha Mayenga (62), uliozikwa eneo la Malindi Mtaa wa Seke uliopo Kata ya Nyahanga Manispaa ya Kahama, ambaye anayedaiwa kuwa aliuawa.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga SACP, Janeth Magomi amesema chanzo cha kifo cha mwanamke huyo ni mgogoro wa ardhi baina yake na mtoto wake na kwamba watu watatu wanashikiliwa kwa ajili ya upelelezi.

Amesema, “tukio hili la kuondoa uhai wa mtu ni la kikatili sana, sisi jeshi la Polisi tutasimamia vizuri upelelezi na tutahakikisha kwamba waliohusika tunawapeleka katika vyombo vya sheria.”

Awali Mwenyekiti wa mtaa wa Seke, Christopher Robart alisema alipewa taarifa na Balozi kuhusu tukio hilo Januari 16, 2025 saa 10 jioni na kutoa taarifa Polisi ambao walifuka kuufukua mwili huo, Januari 17, 2025.

Amesema, “jana majira ya saa kumi nilipigiwa simu na balozi kwamba kuna tukio huku, nilipofika katika eneo hilo tulipewa taarifa na polisi kwamba tulinde eneo hilo ndipo polisi wamekuja leo na kufukua shimo hilo na kukuta mwili wa mwanamke.”

Kwa upande wake Mume wa marehemu Mashauri Mlekwa amesema alipewa taarifa za kupotea kwa mke wake siku ya Jumatatu alipoenda shambani kulima na vijana wake ambao walirudi lakini bibi huyo hakuonekana.

Amesema, vijana hao waliporudi walihamisha vitu vya marehemu na kuuza baadhi ya magunia ya mpunga na mmoja wao aliondoka kwenda Katoro.

Naye mmoja wa mashuhuda, Juma Dutu amesema alipewa taarifa na wachungaji wake wa kwamba Ng’ombe walienda na kuzingira eneo hilo ndipo wachungaji hao walipoenda kuwafukuza na kugundua kuwa kuna kitu kimefukiwa.

“Wachungaji wangu wa ng’ombe walikuwa wanachunga katika maeneo haya ndipo ng’ombe walikimbilia eneo hilo na kuanza kufukua, wachungaji wangu waliwapiga ng’ombe ili watoke ndipo walipogundua kwamba kuna kitu kimefukiwa na kuja kunipa taarifa”, amesema Juma.

Mapigano DRC yatengeneza wakimbizi wa ndani
Habari kuu kwenye Magazeti ya leo Januari 18, 2025