Wafanyabiashara Mkoani Simiyu, wameiomba Serikali kuangalia uwezekano wa kupunguza asilimia ya kodi ya ongezeko la thamani (VAT), ya asilimia 18 kwani imekuwa mwiba kwao na inagusa mitaji yao na hivyo kuwafanya washindwe kumudu kuilipa.

Wakizungumza katika kikao maalum kati yao na Tume ya mlipa kodi iliyoundwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa lengo la kusikiliza kero, maoni, changamoto na mapendekezo ya wafanyabiashara nchini wamesema kodi hiyo inatozwa kibaguzi kwani baadhi yao hawailipi na wengine huuza bidhaa kwa bei ya chini na kuwaathiri wanaolipa.

Mmoja wa Wafanyabiashara hao, Emmanuel Mongo ambaye alizungumza kwa niaba ya wauzaji wa mazao ya misitu mjini Bariadi amesema utofauti ya bei kati ya mfanyabiashara mmoja na mwingine kwa bidhaa za aina moja, imekuwa kikwazo kwani kikawaida mteja hununua bidhaa sehemu yenye bei rafiki.

“Mimi ninauza mbao kwa shilingi elfu 11 lakini silipi VAT yupo jirani yangu anauza ubao ule ule kwa shilingi elfu 13 kwa kuwa analipa VAT, sasa huyu mteja kitu gani kitamfanya aache kununua kwangu akanunue kwa jirani yangu, mwisho wa siku hali lazima iwe ngumu kwa jirani yangu sasa ni bora kote iwe sawa ili tuondoe huu utofauti,” alifafanua Emmanuel.

Aidha, Wafanyabiashara hao wameitaka Serikali kupitia mamlaka zake kukata kodi hiyo tangu kiwandani mahali ambapo bidhaa inazalishwa, ili Wafanyabiashara wote wawe na uwiano sawa na mtumiaji wa mwisho ahusike katika kuchangia mapato hayo.

Wanasema, mlolongo mrefu wa ushuru na kodi kulingana na makadirio ya TRA yamekuwa yakiziumiza sekta nyingi hususan uvuvi kwani ili wailipwe Mfanyabiashara anapaswa kugusa mapato yake ya ndani kutokana na kodi kuwa kubwa kuliko faida ya mzigo kama ambayo katibu wa wavuvi kanda ya Magu Ndalahwa Mabula alieleza.

“Katika ukusanyaji wa samaki kilo elfu mbili natakiwa niwe na shilingi milioni kumi na tisa na efu hamsini na nikiuza napata shilingi milioni kumi na tisa na laki saba TRA wakipiga hesabu zao natakiwa nilipe milioni nane sabini nane kwa mwaka ambayo hata sijaifikia kwa hiyo nikijitahidi kulipa ina maana nilipe kwa pesa za mtaji na si faida,” alibainusha Ndalahwa.

Akijibu baadhi ya malalamiko hayo, Meneja wa Mamlaka ya Mapato Nchini (TRA), Mkoa wa Simiyu, Joseph Mtandika amesema ili kupunguza kiwango hicho kutoka asilimia 18 hadi kwenda chini ya asilimia 10 ni lazima Serikali iongeze wigo kutokana na takwimu kuonesha kuwa hakuna uwiano kati ya idadi ya Watanzania na wafanyabiashara waliopo.

“Tunatakiwa kupanua wigo wa wafanyabiashara waongezeke na wawe na mazingira mazuri kama tunataka kupunguza hii kodi, kwa sababu hii asilimia bado tunaihitaji ukiangalia hadi Desemba mwaka jana (2024) tumesajili wafanyabiashara elfu 42 kati wa Watanzania milioni 68 unaweza kuona utofauti mkubwa uliopo,” Mtandika alisema.

Akitoa hitimisho la mjadala huo, Prof. Mussa Assad amesisitiza kuwa mamlaka zote za Serikali zinapaswa kwa na mifumo ambayo inasomana, ili Mfanyabiashara anapokuwa amefanya malipo basi aweze kuonekana.

Amesema, “mifumo kusomana imezungumzwa siku nyingi sana na ninadhani kuna ubishi fulani kati ya hizi taasisi zenu mnahisi hio mifumo ni mali yenu hapana hiyo ni mali ya serikali fanyeni kwa uwazi ili kazi ziendelee kuwa rahisi zaidi muda wowote taarifa zinapotakiwa zionekane.”

Kwa upande wake Prof. Florens Luoga amewataka Wafanyabiashara kuendelea kutumia njia mbalimbali kutoa maoni ikiwepo simu za viganjani, kuelezea changamoto, mapendekezo na kero zao, ili ziweze kufanyiwa kazi kwa lengo la kuboresha mazingira yao ya kibiashara.

Juni 2024 katika moja ya vikao bungeni jijini Dodoma, hoja ya punguzo la Kodi ya thamani iliwasilishwa ambapo Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba alielezea umuhimu wake katika kutekeleza miradi mbalimbali ya kitaifa na kusema endapo asilimia 2 itaondolewa zaidi ya bilioni sita zitapungua kwenye pato la Taifa na kuathiri miradi hiyo.

Maamuzi ya Ancelloti yawaweka njiapanda mashabiki Real Madrid
Chelsea watuma salamu kuelekea mchezo wa Manchester City