Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa ameapishwa na Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Tanzania, Kanda ya Dodoma, Edwin Kakolaki kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Jeshi la Polisi, Magereza, Zimamoto na Uokoaji na Idara ya Uhamiaji.

Katika uapisho huo uliofanyika hii leo Januari 21, 2025 katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Kituo Jumuishi cha Utoaji wa Haki jijini Dodoma, Jaji Kakolaki pia amewaapisha Kamishna wa Polisi Zanzibar, Kombo Khamis Kombo na Kamishna wa Utawala na Menejimenti ya Rasilimali Watu katika Jeshi la Polisi, CP. Tatu Rashid Jumbe kuwa wajumbe wa Tume hiyo.

Akizungumza mara baada ya uapisho, Jaji Kakolaki amemsisitiza Mwenyekiti wa Tume na Wajumbe kutekeleza majukumu yao kwa ufasini, weledi na kutenda haki kwa mujibu wa Sheria.

“Niwaombe mtekeleze majukumu yenu bila upendeleo wala uonevu lakini mkiwa mnaongozwa na sheria, taratibu, miongozo na taratibu nyingine za kimazoea (busara)” amesisitiza Jaji Kakolaki.

Jaji Kakolaki amemhimiza Mwenyekiti wa Tume na Wajumbe kutimiza wajibu wao kwa wakati ili kuviwezesha Vyombo vya Usalama vilivyochini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kufanya kazi na kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi mkubwa.

Kwa Upande wake, Mwenyekiti wa Tume ya Jeshi la Polisi, Magereza, Zimamoto na Uokoaji na Idara ya Uhamiaji, Innocent Bashungwa amemhakikishia Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Watanzania kuwa Tume itasimamia Sheria na kutenda haki bila kumuonea mtu.

Bashungwa ameeleza kuwa ataiongoza Tume kufanya maamuzi kwa wakati ili kuviwezesha Vyombo vya Usalama kuendelea kutekeleza majukumu yao kikamilifu.

“Vikao tulivyoelekezwa kuvifanya, tutahakikisha hakuna kikao kinavuka muda ambao tumeelekezwa kufanywa, na kufanya hivyo tutaweza kufanya maamuzi kwa wakati” ameeleza Bashungwa.

Tume ya Jeshi la Polisi, Magereza, Zimamoto na Uokoaji na Idara ya Uhamiaji ina mamlaka ya kuajiri, kusitisha, kupandisha cheo na kumthibitisha kazini Askari mwenye cheo kuanzia Mkaguzi Msaidizi hadi Kamishna Msaidizi.

Habari kuu kwenye Magazeti ya leo Januari 22, 2025
Dkt. Biteko ataka Mitaala vyuoni iendane na mabadiliko ya teknolojia