Jumla ya miche laki moja ya aina mbaimbali imetolewa na shirika la Via Viation kupitia mradi wake wa Via Green katika Wilaya ya Magu mkoani Mwanza, ili kuboresha mazingira pamoja na kukabiliana na tatizo la ukataji wa miti katika Wilaya hiyo.
Akizungumza katika zoezi la upandaji wa miti hiyo Mkurugenzi wa shirika hilo, Suzan Mashibe amesema shirika hilo lipo katika mpango wa kupanda miche milioni moja katika maeneo mbalimbali na tayari miche laki moja imetolewa katika wilaya ya Magu.
“Kwa wilaya ya Magu tumeanza na miche 100,000 kati yake miche 5000 tumeleta hapa Mwanza Girls. Tumewaletea miche ya miti ya aina mbalimbali ikiwemo ya matunda, mbao, vivuli na urembo.
“Lengo letu ni kugawa miche milioni moja ya miti kwa mwaka kwenye wilaya mbalimbali za kanda ya ziwa hasa ikizingatiwa jamii za watu wa ukanda huu zinategemea zaidi nishati ya mkaa na kuni katika kupikia,” amesema Suzan.
Kwa upande wake Katibu Tawala wa Wilaya hiyo, Jubileth Hauo ambae amemwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Magu, Joshua Nassari amelipongeza shirika hilo kwa kuendelea kushirikiana na serikali katika kuboresha mazingira huku akiwaomba wadau wengine kujitokeza katika kutoa misaada ya miti ili wilaya hiyo iwe na miti ya kutosha.
“Kama Wilaya tumeandaa miche milioni 1.5 kwa sababu nakumbuka wakati nafika Magu, ilikuwa wilaya ya jangwa… hapakuwa na miti lakini sasa hali ni nzuri, cha msingi tuendelee kustawisha miti,” amesema.
Afisa Maliasili na Mazingira wa Wilayani Magu, Ngusa Buyamba amesema kwa mwaka huu wa 2025 wilaya hiyo imejiwekea malengo ya kupoanda miti milioni moja na laki tano na mpaka sasa wameshapanda jumla ya miti laki saba na thelathini na nane hivyo ni jukumu la kila mwananchi wa wilaya hiyo kuilinda miti ambayo tayari imeshapandwa ili iweze kuja kuleta manufaa hapo badae