Serikali imefunga mifumo ya ki-elektroniki katika ngazi za Mikoa na Wilaya, ili kurahisisha upatikanaji wa hati za safari (pasipoti) na hati za dharura za safari kwa lengo la kuwaondolea usumbufu raia wa Tanzania pale wanapohitaji hati hizo kwa ajili ya kushiriki shughuli za kijamii katika nchi jirani.

Ameyasema hayo Naibu waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Daniel Sillo, hii leo Januari 28, 2025 katika Mkutano wa 18 wa Bunge wakati akijibu swali la Mbunge Jimbo la Kalambo, Josephat Sinkamba aliyeuliza ni lini Serikali itaondoa usumbufu wa kupata vibali na gharama pale raia wa Tanzania wanapolazimika kushiriki shughuli za kijamii nchini Zambia.

“Kwa raia wanaoishi ndani ya eneo lisilozidi kilometa 10 kutoka mpaka wa nchi yetu na nchi Jiranina wananchi wanapokuwa na shughuli za dharura kama vile misiba na magonjwa, hupatiwa ruhusa (vibali) maalum kuwawezesha kwenda umbali usiozidi kilomita 10 ili waweze kushiriki shughuli hizo,” amesema.

“Aidha, kwa wale wanaoenda nchi jirani kwa ajili ya shughuli za kiuchumi, wanapaswa kufuata Sheria na Taratibu za nchi husika katika kulipia vibali vinavyoendana na shughuli wanazoenda kufanya” aliongeza Sillo.

Aidha, amesema Serikali inaendelea kulipa madai ya askari polisi waliomaliza muda wao wa kazi baada ya kustaafu na jumla ya fedha kiasi cha Shilingi Bilioni 97,120,011,700.26 zinadaiwa.

“Mpaka sasa madai yaliyohakikiwa na kuwasilishwa Wizara ya Fedha kwa ajili ya malipo ni shilingi 75,214,744,005.10 ” amesema

“Kwa sasa madai yanayoendelea kuhakikiwa ni ya mwaka wa fedha 2023/2024 na kiasi cha fedha Shilingi Bilioni 21,905,267,695.16 zinadaiwa, na Pindi uhakiki ukikamilika, madai yote yatawasilishwa Wizara ya Fedha kwa ajili ya malipo,” amesema Sillo.

Mpango wa Kitaifa wa Nishati kuzinduliwa - Dkt. Samia
Huduma ya umeme Afrika kuwafikia watu Mil. 300 - Dkt. Adesina