Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema Tanzania ni moja kati ya nchi 12 zitakazozindua mpango mahususi wa kitaifa kuhusu Nishati.

Akizungumza hii leo Januari 28, 2025 katika Mkutano wa Nishati wa Wakuu wa Nchi za Afrika, Rais Samia amesema mpango huo unatarajia kuongeza kasi ya kuunganisha umeme nchini hadi kufikia asilimia 72 ifikapo mwaka 2030.

“Ili kufanikisha azma hiyo ndani ya muda wa miaka mitano ijayo, tutahitaji uwekezaji wenye thamani ya dola za kimarekani bilioni 13, ambapo dola bilioni 5 zitapatikana kutoka sekta binafsi hapa nchini,” amesema Rais Samia.

Aidha, Rais Samia amessma hadi sasa, Tanzania ina uwezo wa kuzalisha megawati 3431 za umeme, ambapo asilimia 58 ya hizo inatokana na vyanzo vya maji, asilimia 35 inatokana na gesi na asilimia saba inatokana na vyanzo vingine.

Amesema, “Shabaha yetu ni kuongeza megawati 2463 za nishati kutokana na nishati ya jua, gesi asilia, upepo, joto ardhi na vyanzo vingine ifikapo 2030.”

Vijana wajiandae kwa soko la ajira - Rais Benki ya Dunia
Mifumo kielektroniki imerahisisha upatikanaji hati za safari - Sillo