Afarah Suleiman, Babati – Manyara.

Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga amemuapisha Mkuu wa Wilaya ya Mbulu, Michael John Semindu aliyeteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan Januari 25, 2025.

Akizungumza na Wakuu wa Wilaya mara baada ya uapisho huo, Sendiga aliwaelekeza vipaumbele vyake katika utendaji wa kazi, ikiwemo ukusanyaji wa mapato ili Serikali iweze kuwahudumia Wananchi wake na kuleta maendeleo katika Taifa.

Alisema, kipaumbele kingine ni usikilizaji na utatuzi wa kero za Wananchi kuanzia Ngazi ya Mtaa mpaka katika Halmashauri zao, kusimamia ulinzi na usalama kwa kuweka mikakati ya kudhibiti Uhalifu, kusimamia usafi wa mazingira ili kuweka Mkoa katika hali ya usafi pamoja na usimamizi, ufuatiliaji na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

“Nendeni  mkatimize wajibu wenu ipasavyo na mkatekeleze  matarajio ya Mhe.Rais Samia Suluhu Hassan kwani amewaamini na ndio maana amewapa nafasi hizo.” alisema Sendiga.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Mbulu, Michael John Semindu ameahidi kufanya kazi kwa ushirikiano na watendaji wenzake pamoja na kuyapokea maagizo yote yaliyoagizwa na mkuu wa Mkoa na kuyatekeleza majukumu yao yote kwa weledi.

Hafla ya uapisho imefanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara mjini Babati na kuhudhuliwa na wakuu wote wa wilaya Tano za Mkoa wa Manyara pamoja viongozi mbalimbali wa Serikali na Vyama vya siasa.

Tanzania, Somalia wasaini makubaliano ulinzi na usalama
Rais Samia aongoza kikao cha dharura SADC-ORGAN