Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa Elimu, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Dkt. Emmanuel Shindika, amewataka Maofisa Elimu wa Mikoa na Wilaya kuendelea kusimamia utendaji wa walimu, ili kufanikisha jitihada za Serikali katika kuboresha elimu.

Akizungumza Mkoani Singida wakati wa kufunga kikao kazi cha tathmini ya utekelezaji wa shughuli za elimu kwa kipindi cha Julai hadi Desemba 2024, Dkt. Shindika amesisitiza umuhimu wa kuimarisha mahusiano mazuri kazini, kuwalipa walimu stahiki zao na kuhakikisha malipo ya likizo yanalipwa kwa wakati.

Ameeleza kuwa pamoja na changamoto ya upungufu wa walimu, hasa katika halmashauri za vijijini, ni muhimu kuhakikisha walimu waliopo wanatekeleza majukumu yao ipasavyo. Pia aliwataka viongozi hao kufanya tathmini ya matokeo ya mitihani ili kubaini changamoto na kuzitatua kwa wakati.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Maofisa Elimu, Mwalimu Juma Kaponda, ameishukuru Serikali kwa jitihada zake katika kuboresha sekta ya elimu na kuahidi kushirikiana na wadau wote kutekeleza maazimio ya kikao hicho.

Wapewa mafunzo utekelezaji mkataba huduma kwa mteja 
Mitungi ya Gesi kwa Bei ya ruzuku: REA waifikia Hai