Ofisi ya Rais-TAMISEMI kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais-Utumishi imetoa mafunzo ya uandaaji wa mkataba wa huduma kwa mteja kwa Makatibu Tawala Wasaidizi Sehemu ya Utawala na Rasilimaliwatu pamoja na Wakuu wa Vitengo vya Mawasiliano Serikalini kutoka ofisi za wakuu wa mikoa.

Akifungua mafunzo hayo mkoani Morogoro, Mkurugenzi wa Tawala za Mikoa, Beatrice Kimoleta, amewataka washiriki kutumia maarifa yatakayopatikana ili kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi kwa ufanisi na uwajibikaji zaidi.

Amesisitiza kuwa mikataba hiyo itawawezesha wananchi kupata huduma bora kwa wakati, huku akiwataka maafisa wa mawasiliano kuhakikisha elimu kuhusu utekelezaji wake inawafikia wananchi kupitia mikutano na semina mbalimbali.

Kaimu Katibu Tawala Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora , Elihuruma Nyella amesema wamepokea maelekezo ya Mkurugenzi Kimoleta, hivyo watahakikisha wananchi wanapata huduma bora kama zitakavyoanishwa kwenye mikataba ya huduma kwa mteja ya ofisi za wakuu wa mikoa nchini.

Naye, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Katavi Ambwene Mwaifuge amesema kuwa, Maofisa Habari wanalo jukumu la kuitangaza mikataba ya huduma kwa wateja kupitia mikutano ya hadhara, mikutano ya dini na semina mbalimbali zitakazofanyika ndani ya mikoa ili mikataba hiyo itumike ipasavyo katika kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Mafunzo haya ya siku nne yanatarajiwa kuwajengea uwezo washiriki katika kuandaa mikataba ya huduma kwa wateja, hatua inayolenga kuboresha huduma za umma nchini.

Kituo cha Forodha Kabanga kutoa huduma saa 24
Tuendelee kusimamia utendaji wa Walimu - Dkt. Shindika