Swaum Katambo, Mlele – Katavi.

Jumla ya madawati 136 yatapunguza uhaba wa Madawati katika shule za Msingi na Sekondari za Wilaya ya Mlele Mkoa wa Katavi na kuwa nyenzo muhimu kwa Wanafunzi kupata mahala pazuri pakujifunzia.

Madawati hayo yametolewa na kampuni ya Premium Active Tanzania ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa sera yake ya kurudisha faida wanayopata kwa jamii kwenye sekta za elimu, afya, maji, mazingira na uongozi hasa maeneo ambayo wanafanya shughuli za kununua zao la tumbaku.

Akikabidhi madawati hayo yenye thamani zaidi ya milioni 9 Januari 30, 2025 kwa Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mlele Beatrice Rumbeli, Meneja wa kampuni hiyo Nicco Roussos amesema suala la upungufu wa madawati ni muhimu kushughulikiwa kwa haraka kwa maendeleo ya elimu.

Akiwa katika shule ya msingi Igombe, Meneja huyo amesema mbali na kutoa madawati pia katika maeneo mengine wametoa Kompyuta, mashine ya kuchapa karatasi na kopi, meza za ofisini na vifaa mbalimbali zenye thamani zaidi milioni 112.

Roussos amebainisha kuwa kwa kuzingatia uzalishaji wa msimu wa kilimo mwaka 2024 kampuni hiyo imeweza kutoa madawati 1000 yenye thamani ya fedha zaidi ya milioni 71 katika wilaya za Tanganyika, Mpanda, Chunya na Songwe.

“Madawati 136 ni sehemu ya madawati 1000, hivyo shule ambazo zimenufaika katika Wilaya ya Mlele ni Wachawaseme, Mgombe, Kamsisi na Inyonga ambapo kila shule imepata madawati 34” amesema.

Meneja huyo ameeleza kuwa utoaji wa vifaa hivyo unazingatia maombi ya kila mnufaika pamoja na kulingana na uzalishaji bora wa zao la tumbaku wa eneo husika.

Meneja Mahusiano wa Premium Active Tanzania Yusuph Mahundi, amesema kuwa wanawajibu mkubwa kama kampuni kusaidia Serikali kwenye mambo muhimu ya maendeleo ya jamii.

Mahundi amefafanua kuwa kampuni hiyo inafanya kazi na vyama vya msingi 50 nchini huku ikitoa fedha za ushuru dola 107,000 na zaidi ya dola 6,000 katika halmashauri zinazolima zao la tumbaku.

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mlele Beatrice Rumbeli, licha ya kupongeza kampuni hiyo amesema msaada huo umekuwa muhimu sana kwenye kukuza sekta ya elimu.

Rumbeli amesisitiza serikali itaendelea kutoa kushirikiana na taasisi mbalimbali zinazounga mkono maendeleo kwenye sekta mbalimbali.

Kaimu Afisa Elimu Msingi Wilaya ya Mlele Peter Nyamafu, ameiomba Premium Active Tanzania kuendelea kutoa misaada ya namna hiyo kwani halmashauri hiyo bado inaupungufu wa madawati 4524.

Ili kuweza kuondoa upungufu huo, Juhudi za lazima zinapaswa kuchukuliwa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kutafuta ufumbuzi wa kuondoa kero hiyo.

Bungeni: Mabadiliko sheria ya ajira kumbeba Mwajiriwa