Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri, ametangaza kukamilika kwa mchakato wa kuandaa Sera ya Taifa ya Maji. S

era hii mpya, inayotokana na mapitio ya Sera ya Mwaka 2002 (NAWAPO 2002), imejumuisha maboresho yanayolenga kuziba mapungufu ya sera iliyopita pamoja na kuakisi maendeleo ya teknolojia na mabadiliko ya tabianchi.

Akihitimisha rasmi Kongamano la 4 la Kimataifa la Kisayansi la Maji, Mhandisi Mwajuma amesema kuwa hatua hii ni mafanikio makubwa kwa Sekta ya Maji nchini. Ameeleza kuwa utekelezaji wa malengo yaliyomo kwenye sera hiyo utasaidia kupunguza changamoto mbalimbali, hususan katika upatikanaji wa majisafi na usafi wa mazingira, usimamizi wa vyanzo vya maji, na kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.

Mhandisi Mwajuma amepongeza mjadala wa kina uliofanyika katika kongamano hilo, akisisitiza kuwa mapendekezo yaliyotolewa ni muhimu kwa mustakabali wa Sekta ya Maji. Amehimiza wadau wote, ikiwemo Serikali, Sekta Binafsi, Mashirika ya Kijamii, na Wadau wa Maendeleo, kushirikiana kikamilifu katika kutekeleza mapendekezo hayo kwa vitendo.

Amesisitiza kuwa changamoto za maji zinahitaji suluhisho za pamoja na za kisayansi, huku akitoa wito kwa wadau kutumia teknolojia za kisasa ili kuboresha huduma za maji na usafi wa mazingira. “Ni wakati wa kuchukua hatua madhubuti kwa pamoja ili kuhakikisha kila mtu anafurahia haki ya kupata maji safi na salama,” Katibu Mkuu amesema.

Aidha, Mhandisi Mwajuma amekiri kuwa mafanikio yaliyopatikana katika Sekta ya Maji yametokana na mchango mkubwa wa wadau wa ndani na nje ya nchi. Ametoa wito kwa wadau wote kuendelea kushirikiana ili kuhakikisha usimamizi endelevu wa rasilimali za maji na upatikanaji wa huduma bora za maji safi na usafi wa mazingira kwa maendeleo ya taifa.

“Sekta ya Maji ni nguzo muhimu kwa maendeleo ya uchumi na ustawi wa jamii. Ni jukumu letu kuhakikisha tunabuni mikakati bunifu na endelevu kwa ajili ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi,” Katibu Mkuu amesisitiza.

Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha Maji, Dkt. Adam Karia, ameishukuru Wizara ya Maji kwa kuendelea kukipa kipaumbele chuo hicho. Akiahidi kuimarisha ubora wa chuo kwa kuboresha mitaala, kuongeza kozi mpya, na kuongeza udahili wa wanafunzi watakaosaidia kuboresha Sekta ya Maji. Aidha, ametangaza kuanzishwa kwa Centre of Excellence in Integrated Lake Management, ambayo itajikita katika kutafuta suluhisho za utunzaji na usimamizi endelevu wa rasilimali za maji.

Kongamano hilo la kimataifa, lililoandaliwa na Chuo cha Maji, limewakutanisha wadau mbalimbali wa Sekta ya Maji ndani na nje ya nchi kujadili changamoto za maji na usafi wa mazingira katika muktadha wa mabadiliko ya tabianchi. Kongamano limehitimishwa kwa wito wa kuchukua hatua za haraka na ushirikiano wa wadau wote ili kukabiliana na changamoto hizo, huku likisisitiza umuhimu wa elimu na uhamasishaji wa jamii kuhusu matumizi bora ya maji.

Mitambo nane Mradi JNHPP imekabidhiwa Serikalini - Biteko.
Ajali ya Basi, gari dogo yauwa Watatu Moshi