Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Khamis Hamza Khamis amesema jumla miti milioni 686.24 iliyopandwa katika halmashauri mbalimbali nchini imestawi ambapo amesema miti iliyopandwa na kustawi ni sawa na asilimia 82.3 ya miti yote milioni 866.7 iliyopandwa katika kipindi cha mwaka 2020/2021 hadi 2023/2024.

Khamis amesema hayo bungeni jijini Dodoma leo Februari 5, 2025 wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu Mhe. Tunza Malapo ambaye alitaka kujua kama Serikali imefanya tathmini ya kujua ni miti mingapi inayopandwa inatunzwa na kukua ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Akijibu swali hilo Naibu Waziri Khamis amesema Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI, imekuwa ikifanya tathmini ya upandaji miti kwa kila mwaka ili kukabiliana na uharibifu wa ardhi, kuenea kwa hali ya jangwa na ukame na mabadiliko ya tabianchi.

Amesema kuwa katika msimu wa mwaka 2024/25 Serikali inaendelea kufanya tathmini ili kubaini idadi ya miti iliyopandwa na iliyostawi kwa maeneo yote nchini.

Aidha, Khamis amedokeza kuwa Serikali inaendelea kuhamasisha wananchi na sekta binafsi kuendelea kupanda miti kwenye maeneo mbalimbali nchini ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi pamoja na kutunza mazingira.

Ametumia nafasi hiyo kutoa wito kwa jamii nzima ya Watanzania kutumia mvua zinazonyesha kipindi hiki kwa kupanda miti katika maeneo mbalimbali ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Akijibu swali la nyongeza la Tunza, kuhusu mkakati wa Serikali wa kuhakikisha miti inatunzwa, Naibu Waziri Khamis amesema Ofisi ya Makamu wa Rais ina maafisa viungo katika mikoa yote ya Tanzania Bara ambao wana jukumu la kufuatilia zoezi la upandaji wa miti.

Khamis ameongeza kuwa pia Ofisi ya Makamu wa Rais inashirikiana na Ofisi ya Rais – TAMISEMI kuhakikisha maeneo ya kando mwa barabara yaliyopandwa miti yanasimamiwa ipasavyo kuhakikisha inastawi.

Vilevile, amebainisha kuwa Serikali ilianzisha kampeni mbalimbali za upandaji wa miti ikiwemo kwenye vyanzo vya maji, kwa wanafunzi wote na kuhamasisha matumizi nishati safi ya kupikia ili kupunguza kasi ya ukataji wa miti kwa ajili ya kuni na mkaa.

Pamoja na hayo pia, amebainisha kuwa, kupitia ziara za viongozi na matukio mbalimbali, Ofisi ya Makamu wa Rais imekuwa ikitumia nafasi hiyo kutoa elimu na kuhamasisha upandaji wa miti kwa kupanda miti katika maeneo mbalimbali.

Akijibu swali la Mbunge wa Pandani, Maryam Omar Said aliyetaka kujua Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha inaongezea nguvu kwa vikundi vya upandaji miti ufukweni, Naibu Waziri Khamis amesema hatua zinazochukuliwa ni pamoja na kutoa elimu kwa wananchi waone umuhuimu wa kupanda mikoko kando mwa bahari.

Pia, amesema Ofisi ya Makamu wa Rais kupitia miradi ya mazingira inawezesha upandaji wa miti hususan aina ya mikoko katika maeneo ya pwani ambayo inasaidia kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.

Itakumbukwa kuwa Serikali ilielekeza na inasimamia zeozi la upandaji wa miti milioni 1.5 kila mwaka kwa halmashauri zote nchini.

Mapenzi yasababisha Gerard Piqué Anamdhihaki Hadharani Iker Casillas
Paul Pogba ahusishwa na Marseille wenyewe wamkataa