Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAKISEMI), Mohamed Mchengerwa, amewataka Wakurugenzi wa Mikoa kote nchini kuhakikisha wanadhibiti matumizi sahihi ya Mfumo wa Kielektroniki wa Ununuzi wa Umma (NeST) ili kuhakikisha unachangia kikamilifu katika maendeleo ya Taifa na ustawi wa wananchi.
Mchengerwa alitoa maagizo hayo katika kikao kazi kilichoshirikisha Mamlaka ya Udhibiti na Ununuzi wa Umma (PPRA), ambapo walihudhuria Wabunge, Wakurugenzi wa Halmashauri, Makatibu Tawala wa Mikoa, Wakuu wa Vitengo vya Ununuzi wa Mikoa na Halmashauri.
Amesisitiza kwamba katika kusimamia matumizi ya Mfumo huo, Wakurugenzi ni lazima wahakikishe utekelezaji wa sheria na kanuni zinazohusiana na ununuzi wa umma unafanyika kwa ufanisi.
Pia amewataka Wakurugenzi kusimamia utekelezaji wa miradi katika Halmashauri zao na kuhakikisha inakamilika kwa wakati. Aliwataka kutumia fedha za miradi kwa ufanisi na kuhakikisha miradi yote, hasa majengo, inakamilika kama ilivyokusudiwa.
Katika hatua nyingine, Mkurugenzi Mtendaji wa PPRA, Denis Simba ameeleza kwamba tangu kuanzishwa kwa Mfumo wa NeST mwezi Julai 2023, zabuni zenye thamani ya zaidi ya trilioni 12 zimepatikana.
Simba ameeleza kuwa Halmashauri ya Kwimba inaongoza kwa matumizi ya mfumo huo, ikiwa na zabuni 2,065, na kuongeza kuwa mfumo huo umeleta mafanikio makubwa katika kudhibiti ununuzi wa umma.