Hali ya upatikanaji wa huduma ya majisafi na salama katika Mji Mdogo wa Karatu ni wastani wa asilimia 75 ikiwa mahitaji ya maji katika Mji huo ni wastani wa lita Mil.8,750,000kwa siku wakati uzalishaji ukiwa ni wastani wa lita 5,919,000 kwa siku.
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Maji Injinia Andrew Kundo wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti maalum, Cecilia Paresso aliyeuliza Je, Serikali ina mkakati gani wa kuondoa tatizo la upungufu wa Maji katika Mji mdogo wa Karatu.
Alisema, “katika kuhakikisha huduma ya maji inakuwa toshelevu kwenye Mji huo, Serikali inaendelea na utekelezaji wa mradi wa maji Bwawani na kwa ajili kunufaisha Kata tatu (03) za Karatu, Ganako na Qurus.”
“Mradi huo umefikia wastani wa asilimia 77 za utekelezaji na unatarajiwa kukamilika mwezi Oktoba, 2025, vilevile katika bajeti ya mwaka wa fedha 2024/25, Serikali itatekeleza mradi wa kuongeza uzalishaji wa maji katika Mji huo kwa kuchimba kisima kimoja pamoja na kuendeleza visima 2 vilivyopo katika eneo la Qorong’aida.”
Hata hivyo, Kundo amesema, kazi zingine zitakazotekelezwa kupitia mradi huo ni pamoja na ujenzi wa tanki la lita 50,000, ukarabati wa matankimanne (04) yenye jumla ya ujazo wa lita 625,000, ununuzi na ufungaji wa dira za maji 2,000.
“Mradi huo utatekelezwa kwa muda wa miezi 18 ambapo unatarajiwa kuanza mwezi Mei, 2025, na mradi huu utakapokamilika sio kwamba changamoto itaisha kwa asilimia 100%, isipokuwa buduma ya upatikanaji wa maji katika mji huo itaongezeka kutoka asilimia 75% mpaka kufikia asilimia 82%.