Madini: Utafiti kuboresha Mazingira ya Biashara Nchini
6 hours ago
Wizara ya Madini, imeweka mkakati wa kuboresha Mazingira ya Biashara nchini baada ya kufanya utafiti wa tozo 66 zinazotozwa na Halmashauri katika shughuli za madini, ikiwemo madini ya dhahabu.
Waziri wa Madini, Antony Mavunde ameyasema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Busanda, Tumaini Magessa aaliyeuliza Je? lini Serikali itapitia upya tozo zilizopo kwenye mnyororo wa uchimbaji na uchenjuaji wa dhahabu zinazowaelemea Wachimbaji Wadogo.
Akijibu swali hilo Mavunde amesema, “tozo zilizobainika katika shughuli za uchimbaji na uchenjuaji wa dhahabu ni pamoja na ushuru wa karasha, ada ya ukaguzi, Vat leaching/CIP, Mialo, ushuru wa kusafirisha miamba ya madini (mbale) na visusi (mabaki ya miamba baada ya kuchenjuliwa (tailings). Mheshimiwa Spika, Aidha, katika kutatua changamoto hizi.”
“Wizara iliitisha kikao Mwezi Agosti, 2024 Mkoani Singida ambacho kilishirikisha Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Wizara ya Fedha, Tume ya Madini, STAMICO, Halmashauri za Wilaya (Ikungi, Chunya, Kahama, Msalala, Meatu, Shinyanga, Mtama na Lindi), FEMATA na TAWOMA,” alibainisha Mavunde.
Waziri wa Madini, Antony Mavunde.
Hata hivyo, amesema rasimu ya Mapendekezo ya Maboresho tayari imeshaandaliwa na ipo katika hatua ya kufanyiwa mapitio na tathmini, ambapo Matokeo ya tathmini hiyo yatasaidia katika kupanga tozo rafiki kwa wachimbaji wadogo.
“Mheshimiwa Spika, kutokana na changamoto za kikodi nchini, Mheshimiwa Rais ameunda Tume ya Maboresho ya Kodi ili ifanye tathmini ya mfumo wa kodi na kuleta mapendekezo ya namna ya kuboresha mfumo wa kodi,” amesema Mavunde.
Aidha ameongeza kuwa, Serikali kupitia Wizara ya Madini imetunga kanuni ambayo inalenga kuhakikisha mwenye leseni na wenye maduara waingie makubaliano ili kuepusha migogoro.
“Kanuni hiyo inapitiwa na wataalamu ikiwa na Lengo la wenye leseni na wamaduara waingie makubaliano ili kuepusha migogoro na sheria inataka kila anaye pewa leseni achimbe yeye asipangishe, na ukikubali kumuingiza mchimbaji mdogo kwenye leseni yako lazima pia huingie nae makubaliano ambapo pia Ndio kanuni hiyo inasema ili tuondoe migogoro hiyo,” alisema.