Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wasira amemtaka Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dk. Pindi Chana kufika wilayani Serengeti kushughulikia suala la mahusiano ya wananchi na Hifadhi ya Serengeti.
Wasira ametoa agizo hili baada ya kupokea kero ya wananchi kuhusu wanyamapori hususan tembo kuvamia makazi na shughuli zao za kilimo na kudai kuwa ni muhimu waziri husika afike Serengeti, ashughulikie tatizo hilo na kutoa ripoti kwa chama kuhusu hatua zilizochukuliwa.
Amesema, “mahusiano ya watu na Tanapa au Gulmet au Ikorongo, hilo nataka kumuagiza waziri wa Maliasili na Utalii aje ashughulikie mahusiano ya watu hao. Kwanza suala la wanyama wanaokula mimea ni Tanzania nzima, hilo sio la Mugumu pekee na li akuwa chanzo cha umasikini kwa Watanzania.”
Wasira ameongeza kuwa, “tunamtaka waziri mwenye dhamana ashughulikie jambo hilo muda mfupi kadiri inavyowezekana na atuarifu ni nini ambacho kinafanywa,” alisema.