Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania – Zanzibar (TAMWA ZNZ), kinatarajia kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Redio kwa kukutana na wadau mbalimbali wa habari ili kutathmini mchango wa redio na mchango wa TAMWA katika kuhabarisha, kuhamasisha
maendeleo na kuchochea mijadala yenye tija kwa jamii.
Hafla hiyo, itafanyika Februari 12, 2025 katika ofisi za TAMWA ZNZ Tunguu na itawakutanisha wadau kutoka sekta ya habari kwa Unguja na Pemba, wakiwemo Viongozi wa vyombo vya Habari, Wahariri, Wakuu wa vipindi, pamoja na Waandishi wa Habari.
Kauli mbiu ya mwaka huu ni “Redio na Mabadiliko ya Tabianchi”, ikilenga kuangazia namna redio inavyoweza kusaidia katika kuelimisha jamii kuhusu athari za mabadiliko ya tabianchi na njia za kukabiliana nazo.
Katika muktadha wa mabadiliko ya tabianchi, redio inachukua jukumu muhimu katika kutoa elimu kwa jamii kuhusu athari za tabianchi, mbinu za kukabiliana nazo, na umuhimu wa uhifadhi wa mazingira. Kupitia vipindi vya redio, jamii inapata taarifa kuhusu mabadiliko ya
hali ya hewa, mbinu za kilimo kinachohimili ukame, na njia za kupunguza uchafuzi wa mazingira.
Aidha kupitia Kaulimbiu hiyo, TAMWA ZNZ inaviomba vyombo vya habari kuandika habari za wanawake na uongozi katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, kwani tafiti za Zanzibar zinaonesha kwamba sauti za wanawake hazipewi nafasi ipasavyo katika vyombo vya habari.
Utafiti uliofanywa na TAMWA ZNZ mwaka 2024 ulionyesha kwamba jumla ya vipindi 2600 viliandaliwa na kurushwa hewani na ZBC na Assalam Radio ambapo kati ya hivyo 11 pekee ndivyo vilivyohusu mabadiliko ya tabianchi ambayo ni sawa na asilimia (0.9%).
TAMWA ZNZ imeeleza kuwa inatambua mchango mkubwa wa wanahabari kupitia redio katika kuhakikisha jamii inapata taarifa sahihi kwa wakati. Redio imeendelea kuwa chombo madhubuti cha kuelimisha jamii kuhusu haki za wanawake na watoto, usawa wa kijinsia, ushiriki wa wanawake katika uongozi, na kujenga uelewa katika katika kukabiliana na vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia.
Kwa ushirikiano wa karibu na vyombo vya habari, TAMWA ZNZ imefanikiwa kutoa jumla ya habari 778 kwa mwaka 2024 kupitia programu mbalimbali na vyombo tofauti vya habari, ambapo kati ya hizo, habari 502, zilichapishwa kwenye mitandao ya kijamii, 120 kwenye magazeti, 101 kwenye redio, na 55 kwenye televisheni.