Viongozi wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Temeke, wamefanya ziara ya kutembelea CCM Wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani, kwa lengo la kujifunza historia mbalimbali za harakati za Uongozi wa TANU hadi CCM, ikiwamo eneo ambalo Muasisi wa Taifa, Mwl. Julias Nyerere alifikia akianza mchakato wa kupata Uhuru.
Viongozi hao, akiwemo Katibu wa vyuo Wanafunzi wa vyuo vikuu, Dua Mkoga ambaye ni kiongozi wa CCM Temeke wamefanya Ziara hiyo ya siku moja kama sehemu ya kuadhimisha kumbukumbu ya Miaka 48 ya kuzaliwa kwa ambaye amesema harakati zao za ukombozi zimeendelea kukifanya CCM kuwa Bora zaidi katika utendaji kazi.
Kwa upande wake Katibu wa Siasa na uenezi kata ya Temeke, Innocent Mahendeka ametaja maeneo mbalimbali waliyotembelea kuwa ni pamoja na ofisi za CCM wilaya ya Bagamoyo, shina la CCM lililoanzia tangu Chama cha TANU maarufu kwa jina la Mti pesa na jengo la Ikulu ya Kwanza ya Africa Mashariki.
Maeneo mengine ni pamoja na yale ya kihistoria ya Machifu kwenye magofu ya kale ya Kaole, eneo la mnara wa TANU ambapo Mwl. Nyerere alikutana na Shehk Ramiya Mji mkongwe na vivutio mbalimbali vya utalii Wilayani humo.
Mzee Mwinyi Akida akizungumzia historia ya eneo hili akimuhusisha Baba wa Taifa Mwl. Julius Nyerere amesema mwaka 1954 alikuja Bagamoyo na alikutana na wazee, ili kuweza kuwapa taarifa za harakati za kupambania ukombozi wa nchi, wakati huo ikiitwa Tanganyika.
Amesema, Mwl. Nyerere akiwa Bagamoyo alikutana na Shehe Lamia ambaye alimshauri wafanye dua maalumu kwa kufunga siku moja ili Mwenyezi MUNGU afanikishe malengo yake ya kutuletea Uhuru wa nchi.
“Baada ya kufanya Dua hiyo Nyerere aliendelea na safari zake za harakati za kupambania uhuru wa nchi yetu ambapo aliendelea kufanya mikutano mbalimbali akielezea azima yake,” alisema Mzee Akida.
Naye Katibu wa Jukwaa la Wanawake Kata ya Azimio wilayani Temeke, Victoria Charles amesema ujio wao Wilayani Bagamoyo ni kujifunza kuhusu Chama cha TANU hadi kupatikana CCM.
Ziara hiyo, imewapa picha kamili ya ni jinsi gani Mwl. Nyerere alifanya katika Uongozi wake na aliahidi kuwaelezea WanaCCM wenzao na makundi mengine umuhimu wa kufika wilayani Bagamoyo ambako kuna historia mbalimbali za kuanza kwa harakati za maendeleo ya nchi.