Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Vijijini, RUWASA inatarajia kusambaza mita za maji za malipo ya kabla (mita za prepaid)baada mafanikio ya kufunga mita za majaribio Kwa wananchi ambazo zimeanza kuonesha mafanikio makubwa.

Akiongea wakati wa ziara ya ukaguzi wa majaribio ya mita hizo mkoani Manyara, Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha na Utawala ya Bodi ya Wakurugenzi RUWASA Aloys Mvuma amesema Bodi ya maji itahakikisha kuwa mradi huo unakua endelevu na msaada zaidi kwa Jamii ili kuweza kufikia matamanio ya utoaji huduma ya maji kama ambavyo imepangwa.

Amesema RUWASA imebuni mbinu hiyo ikiwa na lengo endelevu la kutoa huduma ya maji Kwa wananchi huku ikibainishwa kuwa majaribio ya mita iliyofungwa katika Kijiji Cha Gidas kata ya Gidas inawanufaisha wananchi 4972 ambapo wananchi wanatumia mfumo wa kadi kupata huduma hiyo.

Wananchi wa eneo Hilo ambao wamenifaika na mradi huo wamesema mita hizo zimekuwa na msaada mkubwa kwa jamii ikiwa ni pamoja na kuongeza mapato kwa idara husika kwakua mwananchi analipia huduma ya maji kabla ya kuyatumia jambo ambalo linaondoa ukakasi na mrundikano wa madeni ikilinganishwa na mita za kawaida zilizokuwa zikitumika.

Akitoa taarifa ya hali ya huduma ya maji Kwa Mkoa wa Manyara Meneja wa RUWASA mkoa wa Manyara James Kionaumela amesema upatikanaji wa Maji katika Mkoa wa Manyara ni asilimia 75.5 ambapo Wilaya ya Babati inaongoza kwa upatikanaji wa Maji Kwa asilimia 80.9 na Wilaya ya Kiteto ikiwa nyuma kwa asilimia 64.

Katika hatua nyingine Kionaumela amelezea changamoto kubwa zinazoukabili Mkoa wa Manyara ni pamoja na ukosefu wa usafiri katika Wilaya za Simanjiro na Hanang’ jambo ambalo linapelekea utendaji kazi kutofanyika Kwa wakati.

Aidha , Katibu Tawala Mkoa wa Manyara Mariam Muhaji amesema kuwa Mkoa wa Manyara bado unahitaji huduma ya maji huku akisisitiza kuwa serikali itaendelea kushirikiana na RUWASA kuhakikisha vijiji vyote vinafikiwa huduma ya maji.

Akihitimisha ziara yake aliyoambatana na wajumbe wa Bodi RUWASA Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha na Utawala ya Bodi ya Wakurugenzi RUWASA Aloys Mvuma amesema amepokea changamoto zote zinazoikabili RUWASA mkoa Manyara na kuahidi kuwa atamshauri Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ili apatie ufumbuzi wa changamoto hizo kwa uharaka.

Ushindani wa ajira: Mikakati yapangwa kuwawezesha Vijana
Tanzanite kuuzwa kwenye Masoko ya ndani nje ya Mirerani - Dkt. Kiruswa