Mkutano wa 17 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Nishati, Petroli na Madini la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ulionza Februari 10, 2025 katika Makao Makuu ya Jumuiya hiyo jijini Arusha utafanyika katika ngazi tatu ya Wataalamu Februari 10 -12, 2025, ngazi ya Makatibu Wakuu Februari 13, 2024 na kuhitimishwa katika ngazi ya Mawaziri Februari 14, 2025.
Mkutano huo unatarajiwa kupokea na kujadili taarifa mbalimbali za maendeleo ya sekta ya nishati, petroli na madini katika Jumuiya na kuweka mikakati ya pamoja ya kutatua chagamoto mbalimbali zinazoikabili sekta hiyo ili kuhakikisha nchi wanachama wananufaika kutokana na mchango wa sekta hizo, vilevile kuhakikisha upatikanaji wa nishati ya uhakika, nafuu na endelevu katika Jumuiya.
Ili kufikia adhima hiyo mkutano huo utaangazia agenda mbalimbali ikiwemo; hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa maamuzi ya baraza la hilo la sekta, matumizi ya nishati safi, salama na ufanisi wake, Mkutano na Maonyesho ya 11 ya Petroli ya Afrika Mashariki yanayotarajiwa kufanyika jijini Dar es Salaam Machi 5-7, 2025 na kuhuisha taarifa za utekelezaji wa miradi ya kuunganisha na kusambaza nishati katika Jumuiya.
![](https://dar24.com/wp-content/uploads/2025/02/0-5.jpg)
Mkutano wa 17 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Nishati, Petroli na Madini la EAC ukiendelea katika Makao Makuu ya Jumuiya jijini Arusha.
Akizungumza kwenye ufunguzi wa mkutano huo wa ngazi ya wataalamu Mkurugenzi wa Sekta za Uzalishaji wa Sekretariati ya Jumuiya ya Afrika Mashariki Jean Baptiste Havugimana ameeleza kuwa licha ya mafanikio yaliyofikiwa katika sekta hiyo bado mchango na weledi wa wataalamu wa sekta hizo muhimu katika kukuza uchumi wa Jumuiya unahitajika ili kutatua changamoto zilizopo na hatimaye kufikia malengo yanayotarajiwa na Jumuiya.
Havugimana ametoa rai kwa watalamu hao kujikita katika kujadili na kuyapatia ufumbuzi wa kudumu masuala muhimu yatakayojili katika mkutano huo kwa manufaa ya Jumuiya.
![](https://dar24.com/wp-content/uploads/2025/02/0-6.jpg)
Mkurugenzi wa Sekta za Uzalishaji wa Sekretariati ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Jean Baptiste Havugimana akichangia hoja kwenye Mkutano wa 17 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Nishati, Petroli na Madini la EAC uliokuwa ukiendelea katika Makao Makuu ya Jumuiya jijini Arusha.
Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo wa ngazi ya wataalamu unaongozwa na Abdillah Mataka Mkurugenzi wa Idara ya Miundombinu ya Uchumi na Huduma za Jamii katika Wizara ya Mambo ya Nje Ushirikiano wa Afrika Mashariki na utahitimishwa Februari 14, 2025 katika ngazi ya Mawaziri wanaosimamia Sekta ya Nishati, Petroli na madini umehudhiriwa na wajumbe kutoka Nchi zote saba wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.