Serikali za Tanzania na Misri zimekubaliana kukuza ushirikiano wa kiuchumi kwa maslahi ya pande zote mbili kwa kuimarisha sekta ya usafirishaji, nishati, ujenzi wa miundombinu, uchukuzi, biashara na uwekezaji, kilimo, mifugo na uvuvi.

Makubaliano hayo yamefikiwa wakati Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahamoud Thabit Kombo alipokutana kwa mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri, Badr Abdelatty pembezoni mwa Kikao cha 46 cha Baraza la Mawaziri la Umoja wa Afrika kinachoendelea jijini Addis Ababa, Ethiopia.

Viongozi hao wamejadili juu ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayoendelea kutekelezwa na nchi hizo na kuahidi kuongeza jitihada ya kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati ili kufikia malengo ya miradi husika. Miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa Bwawa la Umeme la Mwalimu Nyerere.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahamoud Thabit Kombo katika picha ya pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri, Badr Abdelatty pembezoni mwa Kikao cha 46 cha Baraza la Mawaziri la Umoja wa Afrika kinachofanyika Februari 12-13, 2025 jijini Addis Ababa, Ethiopia.

Viongozi hao pia, wamezungumzia umuhimu wa kuimarisha usafirishaji na uchukuzi kwa kukuza uwezo wa bandari pamoja na kuwa na usafiri wa uhakika wa majini na reli kwa ajili ya kuruhusu usafiri wa bidhaa, huduma na watu.

Pia wamesisitiza umuhimu wa ushirikiano katika masuala ya elimu pamoja na kuendelea kukuza mpango wa ziara za kimasomo kwa wanafunzi wa mafunzo ya muda mrefu na mfupi ili kukuza uwezo na kujengeana uzoefu katika masuala mbalimbali ya kitaaluma.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahamoud Thabit Kombo akizungumza na Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri, Badr Abdelatty (hayupo pichani) pembezoni mwa Kikao cha 46 cha Baraza la Mawaziri la Umoja wa Afrika kinachofanyika jijini Addis Ababa, Ethiopia Februari 12-13, 2025.

Kupitia mazungumzo hayo suala la kuitishwa kwa mkutano wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Misri limetiliwa mkazo ambapo kumbukumbu zinaonesha kuwa mkutano huo kwa mara ya mwisho ulifanyika mwaka 2018 hivyo wamewasisitiza watalaam wa pande mbili kuhakikisha maandaliziya mkutano huo yanaanza na kukamilika kwa wakati.

Viongozi hao pia wamesisitiza umuhimu wa maonesho ya biashara katika kukuza mtandao wa biashara kikanda na kimataifa pamoja na makongamano ya biashara katika kukuza mtandao wa mawasiliano ya kibiashara.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri, Badr Abdelatty akizungumza na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahamoud Thabit Kombo (hayupo pichani) pembezoni mwa Kikao cha 46 cha Baraza la Mawaziri la Umoja wa Afrika kinachofanyika jijini Addis Ababa, Ethiopia.

Kwa pamoja nchi hizo zimekubaliana kushirikiana katika majukwaa ya kikanda na kimataifa kwa kuunga mkono ajenda zenye maslahi kwa pande zote kwa maendeleo endelevu ya wananchi.

Aidha viongozi hao wameelezea umuhimu wa kuandaa na kufanya ziara za viongozi wa ngazi za juu kwa lengo la kukuza ushirikiano pamoja na kuanzisha ushirikiano katika maeneo mapya.

Mafunzo kwa watoa huduma za Afya kuleta ufanisi wa Chanjo
Arusha: Madereva wawili mbaroni kwa kusababisha ajali, kifo