Serikali kupitia Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa inaendelea na ujenzi wa nyumba 10,000 za makazi ya Jeshi la Wananchi ambapo hadi sasa jumla ya nyumba 6,064 zimejengwa katika Mikoa mbalimbali nchini ikiwa ni utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Miaka Mitano kuanzia Mwaka wa Fedha 2021/22 hadi 2025/26.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa, Bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge, Bakar Hamad Bakar aliyetaka kujua Je, upi Mpango wa Serikali kuboresha Ofisi na Makazi ya Jeshi la Wananchi Nchini.
“Wizara inatekeleza mpango mkakati wa miaka mitano kuanzia Mwaka wa Fedha 2021/22 hadi 2025/26 wa kuliwezesha Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania – JWTZ kuboresha mazingira ya kazi” amesema Bashungwa.
Bashungwa amesema kuwa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Taifa inaendelea na ukarabati wa nyumba 6,064 katika maeneo mbalimbali ya Jeshi la Wananchi, ujenzi wa hospitali kuu ya Jeshi Msalato Dodoma, uboreshaji wa hospitali ya kanda MH Mwanza, na ujenzi wa mabweni ya Maafisa na Askari katika Vikosi na Viteule mbalimbali.
Aidha, Bashungwa amesema Wizara inaendelea na ujenzi wa Makao Makuu ya Ulinzi wa Taifa – Kikombo Dodoma, uboreshaji, na ukarabati wa miundombinu mbalimbali katika Vikosi, Vyuo na Shule.