Naibu Waziri, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Zainab Katimba ameutaka uongozi wa Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo kuwasiliana na Wakurugenzi Halmashauri zote nchini ambazo hazijatimiza maelekezo ya serikali ya kutoa mafunzo ya kuwajengea uwezo viongozi wa serikali za mitaa na vijiji ili wawezeshe kupata mafunzo hayo.
Katimba ametoa maelekezo hayo baada ya kutembelea chuo hicho kilichopo Hombolo jijini Dodoma ikiwa ni ziara ya kikazi ya kutembelea taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Rais – TAMISEMI kwa lengo la kujitambulisha na kuzungumza na viongozi na watumishi wa taasisi hizo ili kupata mwelekeo wa kiutendaji wa Taasisi hizo.

“Mafunzo haya ni ya lazima sio ya hiari mfanye mawasiliano ili waweze kuhakikisha mafunzo haya yanaweza kufanyika kwa wenyeviti wetu hawa na mafunzo haya mnayotoa yana lengo zuri la kuwajengea uwezo wale watendaji wote waliopo huko kwenye mamlaka za serikali za mitaa waweze kutimiza majukumu yao kwa ufanisi,” amesema.

Amesisitiza katika mafunzo ya kuwajengea uwezo viongozi yanatakiwa kuendana na mabadiliko ya kifikra ili mamlaka za serikali za mitaa zielewe kuwa pamoja na utoaji wa huduma kwa jamii bali ni chombo cha kuwezesha shughuli za kiuchumi.
“Mamlaka zetu za serikali za mitaa ziwe ni chombo cha kuchochea na kuwezesha wananchi katika shughuli mbalimbali za uzalishaji mali katika sekta mbalimbali najua mna’component’ nyingi lakini katika eneo hili natoa msisitizo,” amesema Katimba.