Johansen Buberwa – Kagera.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fatma Mwassa amewataka Wananchi na Viongozi mbalimbali wa mkoa huo kutojihusisha na vitendo vya kuruhusu wahamiaji haramu kuingia Nchini.
Mwassa ametoa maagizo hayo kwenye kikao cha Kamati ya Ushauri wa Mkoa (RCC), ambacho kilishirikisha Wabunge, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi, Wenyeviti wa Halmashauri, Vyama vya siasa na Viongozi wengine chenye lengo la kujadili maendeleo ya mkoa huo.
Amesema, kumekuwepo na tabia ya baadhi ya Viongozi wa Kisiasa ya kuwatetea na kuwalinda Wahamiaji haramu kwa maslahi ya kulinda kura zao, kitendo ambacho kinavunja sharia na taratibu za nchi.
“Tumekubaliana kwamba Mkoa kupitia kamati zake za usalama kwa ngazi zote kudhibiti uhamiaji haramu, wawe wanatoka nje ya nchi au ndani wasivamie bila kufuta taratibu kwa maana tumegundua kuna tatizo kubwa ngazi za vitongoji na vijiji,” amesema Mwassa.
Kwa upande wao baadhi ya wajumbe walioshiriki kikao hicho akiwemo, Piusi Ngeze na Mbunge wa jimbo la Muleba Kaskazini, Charles Mwijage wamesema suala la kuondoa wahamiaji haramu si la kusubiri Viongozi wa kitaifa kwani katika maeneo husika vipo vyombo vya ulinzi na usalama ambavyo vitatakiwa kushirikiana na Wananchi kuwadhibiti wahamiaji haramu.