Wakala wa Huduma ya Ununuzi Serikalini (GPSA), umemsimamisha kazi Mayala Mburi, ili kupisha uchunguzi wa tuhuma za utovu wa Nidhamu baada ya kuwajibu vibaya watumishi sita wa Serikali, akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Paulo Chacha.
Taarifa iliyotolewa na Kitengo cha Mawasiliano na Masoko cha GPSA, imeeleza kuwa Mburi anasimamishwa ili kupisha uchunguzi wa tuhuma hizo huku ikimteuwa Stephen Muro kukaimu majukumu ya nafasi hiyo, ili huduma ziweze kuendelea.
“GPSA unalaani na kukemea vitendo vya aina yoyote vya utovu wa nidhamu katika Utumishi ambavyo ni kinyume na Sheria, Kanuni na Taratibu za Utumishi wa Umma. Wakala unaendelea na uchunguzi na hatimaye kuzishughulikia tuhuma hizo kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na Taratibu za
Utumishi wa Umma,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.

Hatua hii inajiri kufuatia tukio la Februari 18, 2025 la Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Paulo Chacha akiwa ameambatana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Tabora kufanya ziara ya kushtukiza katika ofisi za GPSA na kukumbana na kadhia hiyo.
Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Paulo Chacha alimuelekeza Katibu Tawala wa Mkoa huo kumsimamisha kazi Meneja huyo wa Wakala wa Huduma ya Ununuzi Serikalini Mkoani humo, baada ya yeye pamoja na watumishi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu kupiga simu kwa nyakati tofauti majira ya usiku kwa lengo la kuhitaji huduma ya mafuta katika kituo cha serikali wakiwa safarini kuelekea mkoa wa Geita na badala yake Meneja huyo aliwatusi akidai anapata starehe kwa wakati huo.

“Aliwasiliana yeye mwenyewe na watumishi sita kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu wanaenda kwenye tukio kubwa Geita akawambia mkifika mida ya saa mbili au saa tatu usiku mtahudumiwa na bahati mbaya watumishi hao wamefika majira ya saa tatu usiku wakapiga simu kuanzia saa tatu mbaka saa nne simu haijapokelewa.
Badala yake ikaja kupokelewa majira ya saa nne na nusu aliwatukana matusi ya nguoni huyu bwana anawaambia ninyi ni nani mnanipigia simu usiku huu simu, mimi nipo kwenye starehe zangu,” alisimulia RC Paul Chacha.