Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma PPRA imetakiwa kuwa mfano bora wa kusimamia uadilifu katika taasisi za umma nchini, kupitia utekelezaji wa majukumu yake katika sekta ya Ununuzi wa Umma.
Hayo yamesemwa leo Februari 21, 2025 na Naibu Katibu Mkuu Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Xavier Mrope wakati akifungua mkutano wa Baraza la tano la wafanyakazi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi i wa Umma (PPRA) lililofanyika katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julias Nyerere, Kibaha mkoani Pwani.

Amesema watumishi wa umma wanatakiwa kuwa waadilifu muda wote sambamba na kusimamia matumizi ya fedha na mali za umma pindi wanapotoa huduma, hatua ambayo itasaidia kudhibiti matumizi yasio halisi ya fedha na mali za umma.
“Watumishi wa Umma pia mnawajibu mkubwa wa kuepuka vitendo vinavyoweza kushawishi kutenda yaliyo kinyume na maadili wakati mkiendelea na majukumu yenu, watumishi wa umma kwa nchi nzima ni takriban laki sita ambao tunapaswa kutoa huduma kwa zaidi ya wananchi milioni 60, kwa mantiki hiyo naona mlivyo na kazi kubwa ya kulinda maslah ya wananchi,” amesema.

Aidha amesema mabaraza ya Wafanyakazi ni sehemu muhimu sana ya kujadili mambo mbalimbali ikiwemo changamoto za kazini ambayo pia yanachangia kupunguza migogoro na migongano sehemu za kazi na kwamba changamoto zitakazoibuliwa zitazamwe katika mtazamo chanya wa kutatua changamoto zinazowakabili wafanyakazi.
“Mabaraza ya Wafanyakazi ni majukwaa ya kujadili changamoto zenu, kadhalika mnatakiwa kuwa mfano katika utendaji wenu wa kazi endeleeni kutoa maelekezo kwa uwazi yawe sahihi kwa kuzingatia uadikifu,” amesisitiza.

Katika hatua nyengine Mrope alitoa wito kwa Baraza hilo kujadili namna bora ya kuzijengea uwezo Taasisi za Serikali na zisizo za Serikali hatua ambayo itasaidia kupata uelewa kuhusiana na matumizi sahihi ya Sheria ya Ununuzi wa Umma sambamba na kanuni zake za mwaka 2024.
“Kuna mambo mengi mmeanzisha ikiwemo mfumo wa Ununuzi wa Umma wa kieletroniki NeST Kwa lengo la kuimarisha michakato ya ununuzi, hivyo, toeni nafasi kwa wadau wenu wafahamu mifumo yenu vizuri,” alisema.

Awali katika mkutano huo Mkurugenzi wa (PPRA), Dennis Simba amesema tangu kuanza kwa mfumo wa NeST mpaka sasa tayari mfumo huo umeunganishwa na mifumo 20 ili kuendana na malengo ya serikali ya kuhakikisha mifumo inasomana kwa lengo la kuongezaa uwazi zaidi na kurahisisha michakato.
Akielezea Ufanisi wa Mfumo huo, Simba amesema katika tathmini iliyofanyika barani Afrika Mwaka 2024, Mfumo wa NeST ulishinda kwa kupata nafasi ya kwanza katika kategoria ya Ubunifu wa mifumo ya Mamlaka barani Afrika.