Na Boniface Gideon – Tanga.
Wakazi wa Kata ya Kwale Wilayani Mkinga, wamepatiwa Shilingi Milioni 10.5 kwa ajili ya kukopeshana bila riba kupitia vikundi ili kupunguza shughuli za kiuchumi Baharini ambazo husababisha uhalifu, ikiwemo ukataji wa mikoko na uvuvi haramu pamoja na uchafuzi wa fukwe za Bahari.
Fedha hizo zimetolewa na Shirika la Mwambao Coastal Community Network Tanzania mwishoni mwa wiki, ambapo wanufaika watapata fursa ya kuongeza mitaji kwenye Biashara zao.
Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi fedha hizo Mratibu wa Shirika hilo Mkoa wa Tanga Ahmed Salim alisema fedha hizo zimetolewa kwa vikundi 5 vyenye wanachama 150.

“Fedha hizi tunazitoa kwa wanachama 150 ambao tumewafundisha na kuwapatia mafunzo ya Elimu ya Fedha,Utunzaji wa Mazingira hususani Bahari na Rasilimali zake. Lengo la kutoa Fedha hizi,ni kuwasaidia wanachama ni kupunguza shughuli za kiuchumi Baharini kwa kuongeza mitaji ya Biashara zao ili kupunguza utegemezi wa Bahari,” aliongeza Ahmed.
Ahmed alisema fedha hazirejeshwi kwa Shirika hilo bali wanachama waliokabidhiwa wanajiwekea utaratibu wa kukopeshana bila riba,
“Sisi tunakabidhi Fedha kwa Wanachama,hivyo wao wanajiwekea utaratibu wa kukopeshana bila riba ili Fedha hizi ziwepo kwenye mzunguko wa kila siku,tunaamini fedha hizi zitawasaidia Wanachama hawa ikizingatiwa kuwa wengi wao ni Wanachama wa BMU na Maisha yao yanategemea Bahari,hivyo tuna Imani kubwa na Wanachama hawa kuwa watakuwa mabalozi wazuri wa Mazingira.

“Tunaamini kuwa kupitia fedha hizi,mtaongeza vipato vyenu na mtakuwa mabalozi wazuri wa Utunzaji wa Mazingira hususani Upandaji wa mikoko,utunzaji fukwe na uvuvi salama,pia tunaamini kuwa mtakuwa wasimamizi wa Rasilimali za Bahari na kuongeza Vipato vyenu,” alisisitiza.
Kwa upande wake Katibu wa Jumuiya ya za Usimamizi wa Fukwe na Bahari (BMU) kata ya Kwale ,Salehe Kombo,alilishukuru Shirika hilo kwa kutoa Fedha hizo ambazo zimelenga kuwainua kiuchumi wakazi ambao wanategemea Bahari kuendesha maisha yao,
“Tunashukuru sana kwa kupata fedha hizi,hali ya Uhalifu Baharini ni mbaya ,kwahiyo kupitia fedha hizi kila mmoja wetu atakuwa na kazi nyingine nje ya Bahari ,hii itatusaidia kuongeza Vipato vyetu,lakini pia kwasisi tunaofanya doria Baharini tutakuwa wengi zaidi, kwakuwa kila mmoja wetu amepata Elimu ya Mazingira pamoja na faida zake,” alisisitiza Kombo.