Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro linamtafuta dereva wa basi la abiria aina ya Yutong lenye namba za usajili T.975 CSB, mali ya kampuni ya Kasulu Express kwa kosa la kuendesha gari kwa uzembe na kusababisha vifo vya watu wawili.
Taarifa ya Kamanda wa Polisi Mkoani humo, imeeleza kuwa tukio hilo limetokea Februari 26, 2025 saa tano asubuhi katika eneo la kijiji cha Kwambe kilichopo kata ya Dumila, tarafa ya Magore, Wilaya ya Kilosa.
“Gari hilo lililokuwa lililokuwa likitokea Mkoni Kigoma kwenda Mkoa wa Dar es salaam likiendeshwa na dereva ambaye bado anatafutwa liliacha njia na kupinduka na kusababisha vifo vya watu wawili na majeruhi,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.

Aidha, Polisi imesema watu hao wawili waliofariki bado hawajatambuliwa ambao ni mtoto mmoja na mwanamke mmoja, huku miili yao ikihifadhia katika Hospital ya Rufaa Mkoa wa Morogoro kwa ajili ya utambuzi na idadi ya majeruhi inaendelea kufuatiliwa.
Taarifa hiyo imezidi kuarifu kuwa, “uchunguzi wa awali umebaini kuwa chanzo cha ajali hiyo ni pale dereva wa basi alipokuwa analikwepa gari RAE 025D/RL 2423 aina ya FAW kisha kuacha njia na kupinduka.”
Aidha, dereva wa FAW, Munyabungingo Viateur (38), mkazi wa Kigali ambaye alikuwa akitokea Dar es Salaam kwenda Rwanda, amekamatwa kwa mahojiano zaidi.