Na Heldina Mwingira.

 

UKEKETAJI NI NINI?.

Ukeketaji ni kitendo cha kukata sehemu za nje za viungo vya uzazi vya mwanamke, au kwa maana nyingine tunaweza sema ni uondoaji wa sehemu au sehemu yote ya siri ya nje ya mwanamke au kuweka jeraha kwenye viungo vya uzazi vya mwanamke kwa sababu zisizo za kimatibabu.

Kitendo hiki hakina faida za kiafya kwa wasichana na wanawake na ukiukaji wa haki za binadamu za wasichana na wanawake kwani unaweza sababisha kutokwa na damu nyingi na matatizo ya kukojoa na baadaye uvimbe, maambukizo, matatizo wakati wa kujifungua na kuongezeka kwa hatari ya vifo vya watoto wachanga.

WAHANGA.

Zaidi ya wasichana na wanawake milioni 200 walio hai leo wamefanyiwa ukeketaji katika nchi 30 za Afrika, Mashariki ya Kati na Asia ambako ukeketaji unafanyika kwa kiwango cha juu, ambapo mara nyingi hufanywa kwa wasichana wadogo wa umri wa kati ya uchanga na miaka 15.

Kwa mujibu wa ripoti za Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia Watoto na Wanawake – UNICEF,  wasichana zaidi ya milioni mia mbili wanasadikika kufanyiwa Ukeketaji na maeneo ambayo yanayofanya Ukatili wa namna hii ni pamoja na Afrika, Asia na Mashariki ya kati.

Afrika imekuwa na idadi kubwa zaidi ya wahanga wa ukeketaji ikiwa na zaidi ya wanawake milioni 144, mbele ya Asia milioni 80 na Mashariki ya Kati milioni sita, kulingana na utafiti wa nchi 31 kama vile Gambia, Guinea na Somalia ambako kunafanyika ukeketaji.
Ongezeko hilo limechangiwa na ukuaji wa idadi ya watu katika nchi fulani lakini ripoti hiyo pia iliangazia maendeleo yaliyopatikana katika mapambano dhidi ya ukeketaji kwenye maeneo mengine.

TAKWIMU.

Vilevile, Takwimu zinaonesha kuwa asilimia 10 ya wanawake wenye umri wa kati ya miaka 15-49 wamekeketwa hii ni kwa mujibu wa takwimu za demografia ya Afya za mwaka 2015, ilihali takwimu za mwaka 2022 zinaonesha idadi hiyo imepungua kwa asilimia 2 tu ambapo kwa sasa ni asilimia 8 ya wanawake wa umri huo wamekeketwa.

Takwimu hizi pia zinaonesha kuwa mikoa inayoongoza kwa ukeketaji Tanzania ni Arusha,asilimia 43, Manyara (43), Mara asilimia 28 na Singida 20, japo, kuna mikoa ambayo awali haikuwa na ukeketaji lakini takwimu mpya zinaonyesha kuanzia mwaka 2022 wameanza kufanya ukeketaji.

SHERIA.

Katika harakati za kuondoa ukeketaji kwa wasichana, mwaka 1998 Serikali ilipitisha sheria iliyofanya ukeketaji kuwa kosa la jinai hivyo yamepungua kutoka asilimia 18 mpaka asilimia 10.

Mpango wa Taifa wa Utekelezaji wa kukomesha Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (NPA-VAWC) 2017/2021, 2021/2022) umeeleza kwamba ukeketaji ni mila potofu inawapa athari wanawake na watoto. Nchi ya Tanzania imedhamiria kukomesha ukeketaji, kama sehemu ya utekelezaji wa ajenda ya Maendeleo Endelevu ya 2030.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Idadi ya watu duniani, UNFPA, Dkt. Babatunde Osotimehin amesema licha ya mafanikio katika kupambana na ukeketaji wa wanawake na watoto wa kike, bado kuna changamoto kubwa kukabiliana kabisa ukatili huo.
Akizungumza katika mahojiano maalum na Radio ya Umoja wa Mataifa, Dkt. Babatunde ametaja ukeketaji unaonekana ni ajira mbadala yaani ni njia ya kujikwamua kiuchumi.

MTAZAMO.

Miongoni mwa nchi ambazo ukeketaji wanawake na watoto hufanyika ni pamoja na Tanzania ambapo Mwakilishi wa kudumu wa nchi hiyo katika Umoja wa Mataifa, Balozi Tuvako Manongi amesema kwasasa kinafanyika kwa siri zaidi na hivyo hiyo ni changamoto ndani ya mafanikio, ambapo mtazamo wa jamii unazingatia tamaduni zake na huwa mtazamo wake kuhusiana na Ukeketaji dhidi ya wanawake na watoto

Katika kuangazia mitazamo ya jamii Bi. Leilah alipoongea na Dar24 Media alielezea namna ya jamii yao ilivyokuwa ikimtazama mtu asiyekeketwa alisema, “mwanamke asipokeketwa ina tafsiri ya uchafu, pia ilikuwa ni kosa kukaa na mtu asiyekeketwa katika shughuli za kijamii, na ikitokea asiyekeketwa kavaa kiatu aliyekeketwa, yule aliyekeketwa hawezi kurudia kukivaa hiko kiatu, ikitokea amepika chakula wanatia matope, hata ikitokea umekosea unaonekana umefanya kosa husika kwasababu hujakeketwa.”

Anazidi kufafanua kuwa, kabila lao ikitokea msichana asiyekeketwa amepata mimba akijifungua walikuwa wanatupa mtoto labda asijifungulie nyumbani kwao. “Mtoto wa asiyekeketwa anatupwa mara baada ya kuzaliwa kwasababu msichana asiyekeketwa hana thamani katika jamii,” anafafamua Leila.

SABABU.

Ukeketaji mara nyingi huchukuliwa kuwa sehemu muhimu ya kulea msichana, na njia ya kumtayarisha kwa utu uzima na ndoa, ingawa sababu zinazofanya ukeketaji ufanywe hutofautiana kutoka eneo moja hadi jingine ikiwa ni pamoja na mchanganyiko wa mambo ya kitamaduni katika familia na jamii.

Dar24 tumeangazia sababu ambazo hupelekea Ukeketaji dhidi wanawake na watoto kuendelea kushamiri licha ya juhudi zinazofanyika, ambapo Irene Wambura Mwanamke mwenye asili ya kabila kikurya alisema, ” Ukeketaji umekuwa kama biashara mtoto anapewa zawadi baada ya kufanyiwa ukeketaji, kwa hiyo binti anakuwa na kimuhemuhe cha kufanyiwa ili apewe zawadi kama wenzake.”

“Kwa upande wa wazazi, wana tabia ya kurudishiana fadhila, mtoto wa jirani akikeketwa anapewa zawadi kama vile ng’ombe kwa hiyo na yeye binti yake akikua lazima amfanyie ukeketaji ili zawadi zirudi,” anasema Irene.

Tulimtafuta pia Ngariba mstaafu, ambaye aliacha kukeketa baada ya kupata njia ya nyingine ya kujikwamua kiuchumi, hapa anatupa mbinu wanazotumia kukamilisha zoezi hilo akisema, “Kijana wa kiume anamkalia kwenye tumbo au kifuani ili kumdhibiti akiwa anataka kukimbia au kusumbua akiwa anafanyiwa ukeketaji na muda wa kusafishwa baada ya ukeketaji kwasababu kunakuwa na maumivu makali.”

Aidha, ameelezea sababu zilizokuwa zinamfanya afanye kazi ya ungariba, “Mimi nilikuwa nakeketa ili niweze kujikwamua kiuchumi kwa sababu nilikuwa nalipwa sh 100,000 kwa msichana ambaye tayari ameshiriki ngono na sh 30,000 kwa msichana ambaye ni bikra na kuongeza kuwa, yeye amekeketa mabinti wengi ila hajaona faida au kinachoongezeka zaidi ni kutunzwa na fahari tu.

Hata hivyo, aliyefanyiwa ukeketaji jina lake limehifadhiwa alisema kuwa baba yake ndiye alisisitiza, “alisababisha na kuwaambia mangariba kata chote unabakisha cha nini? Nilipohoji kwanini nafanyiwa ukeketaji Nikaambiwa inanisaidia nisiwe muhuni. niliumia sana yaani mzazi wangu anashiriki kunifanyia ukatili, inauma.”

AINA ZA UKEKETAJI.

Ukeketaji umegawanywa katika aina kuu nne ambazo ni (i) uondoaji wa sehemu au kinembe chote (sehemu ya nje na inayoonekana ya kisimi, ambayo ni sehemu nyeti ya sehemu ya siri ya mwanamke), na/au mkunjo wa ngozi unaozunguka sehemu ya siri ya mwanamke na (ii) ni uondoaji wa sehemu au kisimi chote na labia ndogo (mikunjo ya ndani ya uke), pamoja na au bila kuondolewa kwa labia kubwa (mikunjo ya nje ya ngozi ya uke).

Aina ya (iii) inajulikana kama ‘infibulation’, yaani ni kitendo cha kupunguza kwa mwanya wa sehemu ya uke kupitia utengenezaji wa muhuri wa kufunika sehemu hiyo. Muhuri huundwa kwa kukata na kuweka upya labia ndogo, au labia kubwa, wakati mwingine kwa kushona, na au bila kuondolewa kwa kisimi/kinembe.

Aina ya mwisho yaani (iv)  inajumuisha taratibu zingine zote zenye madhara kwa sehemu ya siri ya mwanamke kwa madhumuni yasiyo ya matibabu, kama kutoboa, kuvuta, kuchanja, kukwarua na kuchoma sehemu za siri.

ATHARI.

Ukiachana na athari za kutoka damu nyingi wakati wa kujifungua na kifo, zipo athari ambazo mara nyingi haizungumziwi kwa upana, ambapo mmoja wa Wananchi alisema hajisikii ladha nzuri kufanya tendo la ndoa na mpenzi wake aliyekeketwa akisema, “napata tabu kumuandaa ili tushiriki tendo hawana ladha yoyote hawashughulishi katika tendo lile najiona nimepata mzigo.”

Tuwaelimishe mangariba kwamba kuna njia nyingine ya kisomi ya kumfanya mwanamke asiwe mzinzi sio lazima akatwe kiungo wakielewa wao watatusaidia kuelimisha mabinti na jamii kwa ujumla” alisema Jesca Msambatavangu Mbunge wa Iringa mjini alipohojiwa na Dar24

Akaongeza na kusema, “Nimeongea kwa uchungu kwasababu anayekeketwa ni mwanamke mwenzangu halafu nina experience hivi aliyekeketwa atakuwa hafeel kama ninavyofeel mimi nikiwa katika activity fulani.”

Lakini athari kuu ni pamoja na maumivu makali, kutokwa na damu nyingi (kuvuja damu nyingi), uvimbe wa tishu za viungo vya uzazi, homa kali, maambukizi ya magonjwa kama pepopunda, matatizo ya mkojo, matatizo ya uponyaji wa jeraha, kupata mshtuko na hata kifo.

HATUA MUHIMU.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na wenye Mahitaji Maalum, Dorothy Gwajima anasema, “Kuanzisha madawati ya ulinzi na usalama wa mtoto katika shule za msingi na sekondari ili kutumia jukwaa hilo kuelimishana kuhusu ukeketaji. Vyombo vya habari kuweka kufuatilia, kuweka utafiti na kuona kiasi gani tunaweza kushirikiana kwa pamoja Kutoa mapambano ya dhati dhidi ya mila hii ya ukeketaji inayoleta madhara makubwa kwa wanawake.”

Hivyo, ni jukumu la wadau mbalimbali taasisi zisizo za kiserikali, wanaharakati na mtu mmoja mmoja kushirikiana na serikali katika kuhakikisha ukeketaji dhidi ya watoto wa kike na wanawake unatokomezwa kwani hata Shirika la afya duniani (WHO) linapinga aina zote za ukeketaji, na linapinga watoa huduma za afya kufanya ukeketaji.

WHO inasema, Matibabu ya matatizo ya kiafya yatokanayo na ukeketaji katika nchi 27 zenye maambukizi makubwa yanakadiriwa kugharimu dola za Kimarekani bilioni 1.4 kwa mwaka na inakadiriwa kuongezeka hadi dola bilioni 2.3 ifikapo mwaka 2047 ikiwa hakuna hatua zitakazochukuliwa.

HITIMISHO.

Kiuhalisia, ukeketaji hauna faida zozote za kiafya, na unadhalilisha wasichana na wanawake kwa njia nyingi. Unaharibu uke wa mwanamke na huingilia utendakazi wa asili wa miili ya wasichana na wanawake, ingawa aina zote za ukeketaji huhusishwa na ongezeko la hatari ya matatizo ya kiafya, hatari ambayo ni kubwa zaidi kutokana na aina kali za ukeketaji.

Kwa kuzingatia kazi ya miongo iliyopita, mwaka wa 1997, WHO ilitoa tamko la pamoja dhidi ya mila ya ukeketaji kwa kushirikiana na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto (UNICEF) na Shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu (UNFPA).

Tangu 1997, juhudi kubwa zimefanywa kukabiliana na ukeketaji, kupitia utafiti, kufanya kazi ndani ya jamii, na mabadiliko katika sera za umma na ikumbukwe pia mwaka 2022, WHO itazindua mwongozo wa mafunzo juu ya mawasiliano yanayomhusu mtu binafsi.

Aidha, mbinu ya ushauri ambayo inawahimiza watoa huduma za afya kupinga mitazamo yao inayohusiana na ukeketaji na kujenga ujuzi wao wa mawasiliano, ili kutoa ushauri nasaha wa kuzuia ukeketaji, pia inatakiwa kutolewa.

Wakutana kujadili udhibiti Vijana waporaji Machinjioni Kibaha
Maisha: Ilibaki kidogo nimpoteze mpenzi wangu