Uwepo wa baadhi ya Vijana wanaojihusisha na vitendo vya kupora watu na kuwanyang’anya pesa na simu, hasa nyakati za usiku kwenye Mtaa wa Machinjioni Halmashauri ya Mji wa Kibaha Mkoa wa Pwani, kumeendelea kuwa tishio juu ya usalama wa Wananchi wa maeneo hayo.
Inaarifiwa pia kuwa, ingawa baadhi ya wazazi wa Vijana wanaojihusisha na vitendo hivyo kutambua uovu huo, lakini wamekuwa hawako tayari kutoa ushirikiano na vyombo vya usalama, ili kudhibiti hali hiyo na badala yake wamekuwa wakiwalinda jambo ambalo linaleta maswali yasiyokuwa na majibu.
Hayo yamebainika February 27,2025 wakati wa mkutano wa wakazi wa Mtaa huo uliokuwa na lengo la kujadili masuala mbalimbali ya KImaendeleo.

Baadhi ya wakazi wa Mtaa wa Machinjioni Kata ya Tangini Halmashauri ya Mji wa Kibaha Mkoa wa Pwani, wakiwa kwenye Mkutano wao.
Polisi Kata wa Kata ya Tangini, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Haruna Msoke amesema ili kudumisha ulinzi na usalama wa Mtaa huo kuna ulazima wa wananchi kutoa ushirikiano kwa kila hatua ikiwemo kuwafichua vijana wanaojihusisha na vitendo hivyo na wanaume kushiriki kwenye ulinzi shirikishi.
“Hali ya usalama ndani ya Mtaa huu ni mbaya inatisha na hili limechangiwa na baaadhi ya wazazi kutowadhibiti Vijana wao wanaojihusisha na vitendo vya uporaji na hawaelewi kuwa leo wanawaonea huruma lakini wengine hawatawaonea huruam pindi watakapowakamata” amesema.
Amesema, suala la ulinzi ni la kila raia kwa mujibu wa sharia za nchi na ikibainika kuna watu wanafumbia mamcho vitendo hivyo wanweza kuunganishwa kwenye kundi la uharifu.
“Kwa leo sitazungumza sana kwakuwa idadi ya wananchi ni ndogo lakini nawaomba wanaume tujitokeze kuunda vikundi vya ulinzi shirikishi ili kudumisha amani na usalama kwenye mitaa yetu na kabla ya kuanza shughulu hiyo tunawapa mafunzo maalumu yatakayowawezesha kufanikisha kazi hiyo,” amesisitiza.
Mwenyekiti wa Mtaa huo, Aidan Mchiwa ametaja mikakati iliyopo juu ya kuimarisha ulinzi ndani ya eneo hilo ni pamoja na kuunda vikundi vya ulinzi shirikishi vitakavyokuwa vinafanya kazi kwa kuzingatia sharia zilizopo.
“Suala la ulinzi ni muhimu sana kwa usalama wa Mtaa na hili tutaliwekea kipaumbele kwa kuongeza vijana na kuwasajiri ili watambulike kabla ya kaunza kazi hiyo kikubwa zaidi niwaombe wakazi wa mtaa huu tujitokeze pindi tunapowaita kwenye mikutano,” amesema.
Kwa upande wake Veronica Samuel, mkazi wa Mtaa huo amewataka wazazi na walezi kuwa karibu na watoto wao has waanfunzi wa shule za msingi kwa kuwapa malezi bora jambo litakalowezesha kuzalisha kizazi bora na chenye maadili yanayokubarika.
“Wazazi tujitahidi kuwatunza watoto wetu na kuwafuatilia kwa kila hatua hali hiyo itawezesha kujua usalama wao,” amesema.