Mkazi wa Kijiji cha Kijiweni, Wilaya Sengerema, mkoani Mwanza, Masele Maganga (42) amehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela baada ya kukutwa na hatia ya kumbaka mtoto wa miaka sita ambae jina lake limehifadhiwa kwa sababu za kisheria.
Hukumu hiyo imesomwa na Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Wilaya ya Sengerema, Evod Kisoka mbele ya Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Nyamhanga Tissoro Katika kesi hiyo ya Jinai namba 22850/2024 .
Awali, Mwendesha Mashtaka aliieleza Mahakama kwamba mshtakiwa alitenda kosa hilo Julai 25, 2024, katika Kijiji cha Kijiweni, wilaya ya Sengerema, mkoa wa Mwanza kinyume na vifungu vya 130(1)(2)(a) pamoja na kifungu cha 131(3) cha sheria ya kanuni ya Adhabu sura ya 16 marejeo ya mwaka 2022.
Mshtakiwa alifikishwa Mahakamani kwa mara ya kwanza tarehe 12.07.2024 na kusomewa shtaka hilo ambapo alikana kutenda kaso la kumbaka mtoto huyo.
Upande wa Jamhuri ulileta mashahidi na shauri lilianza kuunguruma katika mahakama hiyo hadi tarehe 19 Februari ambapo mshitakiwa alijitetea akiwakilishwa na Wakili wake msomi Freddy Gervas huku akikanusha vikali kutenda kosa hilo.
Baada ya Mahakama kupitia vifungu vya sheria sambamba na ushahidi uliowasilishwa na upande wa Jamhuri ikiwemo ripoti ya Mganga aliyemfanyia uchunguzi mtoto huyo, pamoja na cheti cha kuzaliwa cha mhanga, Mahakama imejiridhisha kuwa upande wa Jamhuri wameweza kuthibitisha shitaka bila ya kuacha shaka kwamba mtuhumiwa alitenda kosa hilo.
Baada ya kutiwa hatiani mshtakiwa aliiomba Mahakama imuachilie huru kwa kuwa ni mkosaji wa mara ya kwanza na kudai kuwa alipitiwa na shetani.
Akisoma hukumu hiyo Hakimu, Kisoka alimuhukumu mshtakiwa kutumikia kifungo cha miaka 30 jela ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia kama ya Masele.