Serikali imetoa mkopo wa zaidi ya shilingi Bilioni 1 kwa vikundi 60 vya wanawake, Vijana na watu wenye ulemavu katika Halmashauri ya Wilaya ya Ilemela Mkoani Mwanza, ikilenga kuboresha uchumi wa Wananchi.

Akikabidhi mfano wa hundi kwa vikundi hivyo, katibu tawala wa Wilaya ya Ilemela, Wakili Mariam Msengi aambaye alimwakilisha Mkuu wa Wilaya hiyo, Hassan Masala amesema mikopo hiyo ilisimama kwa muda kufuatia mapungufu kadhaa yaliyojitokeza.

“Fedha hizi mkazitumie kama ilivyokusudiwa, serikali inatamani kuona fedha hizi zinawainua kiuchumi, fedha hizi zitumike kuboresha hali zetu za kiuchumi, tutakapowatembelea basi tukute mmenyanyuka kiuchumi hilo ndio lengo la kwanza,” alisema wakili Mariam.

Akiwasilisha taarifa ya utoaji wa mikopo hiyo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, Ummy Wayayu amesema wamezingatia taratibu zote na vikundi 39 vya wanawake vimeidhinishiwa shilingi milioni 618.60, vikundi 17 vya vijana shilingi milioni 492.90 na vikundi 4 vya watu wenye ulemavu  shilingi milioni 24 na vikundi 32 vilivyokidhi vigezo vitapewa awamu inayofuata.

Kwa upande wao baadhi ya wawakilishi wa vikundi vya wanawake, Vijana na wenye ulemavu, Specioza Alex, Jackson Kalunga na Yohana wameishukuru serikali kwa kurejesha utoaji wa mikopo hii ya asilimia 10  na kuahidi  kwenda kuitumia kwa malengo yaliyokusudiwa na kuirejesha kwa wakati, ili na vikundi vingine viweze kunufaika.

Utekeleza miradi mikubwa ya ujenzi wa barabara DMDP waanza DSM
Kijana aomba msaada wa matibabu kuokoa maisha yake